Maabara ya hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila imeingia katika orodha ya maabara zinazotoa huduma bora duniani baada ya kupata ithibati ya ubora ISO 1589:2012 kutoka katika shirika la Viwango vya Ukaguzi Kimataifa kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADCAS).
Mkurugenzi mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Lawrence Museru amesema ithibati hiyo inatokana na SADCAS kujiridhisha na ubora wa vipimo kwa mujibu yanayotolewa na maabara hospitalini hapo. Waliangalia na kuthibitisha vitu mbalimbali ikiwemo ufanisi wa vifa tiba na miundombinu ya maabara kwa aina 17 za vipimo.
“Vipimo vilihakikiwa ili kujiridhisha kubainika vimekidhi viwango vya kimataifa na kama inavyoelekezwa na ISO 1589:2012, ithibati hii itakuwa na faida kwa taifa na hospitali kwani vipimo na majibu yatatambulika kimataifa, kuaminika kwa ubora wa vipimo na majibu kimataifa, pia maabara itakua kituo cha mafunzo na utafiti wa vimelea mbalimbali kutokana na ubora wa huduma” alisema Profesa Museru.
Pamoja na hayo Profesa Museru anasema hospitali hiyo itaendelea na mpango kazi kuhakikisha huduma zinaendelea kuboreshwa zaidi ili kuongeza wigo wa vipimo vyenye ithibati katika mwaka wa fedha 2022 hadi 2023.