Mahakama ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Vincent Wilson Nsumira (21)mkazi wa Kijiji cha Mkesha wilayani Kasulu baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 17 anayesoma Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Nyakitonto.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 13, 2026 baada ya kukutwa akiwa ameoa mwanafunzi huyo, kitendo kilichofuatiliwa na vyombo vya sheria na kusababisha kukamatwa kwake.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na mashahidi sita wa upande wa Jamhuri pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani.
Wakili wa Serikali, Richard Mzule aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa akieleza kuwa vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto na wanafunzi vinahitaji kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo.


