Lugha gongano shuleni ipatiwe ufumbuzi

HomeKitaifa

Lugha gongano shuleni ipatiwe ufumbuzi

Wabunge wa Tanzania wameeleza maeneo mbalimbali yanayohitaji maboresho kwenye sekta ya elimu nchini ikiwemo lugha itumikayo kufundishia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

Baadhi ya wabunge wamependekeza kutumika kwa lugha ya Kiswahili kwa masomo yote isipokuwa tu somo la lugha ya kiingereza huku wengine wakipinga pendekezo hilo.

Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum Kilimanjaro alisisitiza kuwa Kiingereza kisiondolewe bali kifundishwe kuanzia darasa la kwanza. Ameongeza kuwa baada ya kupata elimu wahitimu wwanapaswa kuwa na uwezo wa kuitumia popote waendapo kwa maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Prof. Kitila Mkumbo akasisitiza kuwa ni vyema kama nchi ikapambana na kutatua tatizo la wanafunzi kutokujua lugha zote mbili badala ya kutaka kukimbia lugha moja na kuendelea na nyingine.

Amesisitiza kuwa mwanadamu hujifunza lugha yoyote ile endapo atafundishwa vyema na kuongeza kuwa kukikimbia Kiingereza kwa sababu tu si lugha yetu na wanafunzi huelewa Kiswahili zaidi ni woga. Wapo wanafunzi ambao wanamaliza elimu ya msingi inayofundishwa kwa lugha ya Kiswahili na hawajui kusoma wala kuandika na kuiongea vizuri lugha hii.

Baadhi ya wabunge pia akiwemo Bernadette Mwashashu wameshauri somo la ujasiriamali lifundishwe kwa wanafunzi.

Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti Mbunge, Stanslaus Nyongo kama mwenyekiti pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wamepokea maoni hayo na kuahidi kurejea na majibu mazuri ya kuhakikisha ubora wa elimu unaimarika.

error: Content is protected !!