Madalali wasema wataendelea kuchukua kodi ya mwezi

HomeKitaifa

Madalali wasema wataendelea kuchukua kodi ya mwezi

Jana (Novemba 15,2021) Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi alipiga marufuku madalali wa nyumba kuchukua kodi ya mwezi mmoja kutoka kwa wapangaji kama malipo ya kuwatafutia nyumba. Waziri Lukuvi alielekeza kwamba madalali walipwe na wenye nyumba.

Click Habari iliwatafuta madalali kadhaa wanaofanya shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ili kupata maoni yao kuhusu suala hilo.

Esau John anayefahamika kama Dalali Maarufu, ambaye hufanya kazi zake maeneo ya Mbezi Beach na Salasala, alisema tamko hilo la Waziri Lukuvi ni jema sana na lina nia ya kusaidia Watanzania walio wengi.

Hata hivyo Esau alihoji “Unadhani wenye nyumba wangapi watafuata maelekezo hayo? Si itabidi niendelee kuchukua hela kwa mtu aliyenitafuta mimi nimfanyie kazi ya kutafuta nyumba?”

Dalali Maarufu amesema, kama mwenye nyumba atamtafuta ili amtafutie wapangaji, baasi mwenye nyumba atapaswa kumlipa baada ya kufanikisha kazi yake, lakini kama anayemtafuta ni mpangaji, inabidi waelewane kuhusu malipo.

Dalali mmoja kutoka Sinza ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake amesema, kwa mazingira ya Dar es Salaam ni ngumu mtu kujitafutia nyumba mwenyewe na pia ni ngumu kwa wamiliki wengi wa nyumba kutafuta wapangaji kwa ajili ya nyumba zao.

Lakini amesema, madalali wengi huweza kupata taarifa juu ya chumba ya nyumba iliyo wazi, na hivyo wakaanza kushindana kutafuta mteja wa kupangisha hapo.

“Mwenye nyumba ananilipaje wakati hajanipa kazi mimi nimesikia juu kwa juu? Wewe mpangaji ndiye umenitafuta ukataka nikufanyie kazi, kwa hiyo lazima unilipe wewe kwa sababu saa nyingine nafanya na kazi ya ‘kumuimbisha’ mwenye nyumba akupangishe hata kama kuna mtu mwingine alishawahi hapo lakini kachelewa kulipa” amesema Dalali huyo.

Naye Maliki Muhaji ambaye ni Dalali katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kinondoni, amesema “Sio mara ya kwanza Waziri kuongea kitu cha namna hiyo. Lakini hayo mambo wanaongea tu hayasimamiwi. Walishasema watu wasilipishwe kodi za mwaka au miezi sita lakini bado kuna nyumna nyingi tu hupangishwi bila kodi ya mwaka. Hata hii itakuwa ivyo tu, utaratibu utaendelea ule ule labda kama wataleta watu wa kusimamia kila nyumba”

Tamko la Waziri Lukuvi limepokelewa vizuri na watu wengi, wakisema ni jambo lenye tija.

Hata hivyo, kuna hofu kuhusu usimamizi wa jambo hilo kwani, huku wengine wakihofu kwamba huenda likafanya baadhi ya wenye nyumba kuongeza kodi ili wawalipe madalali.

error: Content is protected !!