MAHAKAMA: Mkataba wa uwekezaji bandarini ni halali

HomeKitaifa

MAHAKAMA: Mkataba wa uwekezaji bandarini ni halali

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imeamua kwamba mkataba wa uwekezaji (IGA) kwenye Bandari za Tanzania ulioingiwa baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai haukuvunja Katiba ya Tanzania wala sheria nyingine yoyote hapa nchini na hivyo ni mkataba halali.

Hukumu hiyo imehitimisha sintofahamu ya zaidi ya miezi miwili iliyokuwa imeikumba nchi tangu Bunge la Tanzania liridhie mkataba huo ambao utaiwezesha kampuni ya DP World kuja kuwekeza katika bandari za Tanzania na kuongeza mapato katika eneo hilo nyeti kwa ukuaji wa uchumi wa taifa.

Majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo iliyofunguliwa na Watanzania wanne waliokuwa wakipinga mkataba huo kwa maelezo kuwa unavunja sheria na Katiba ya Tanzania na kuitaka Mahakama iutangaze kuwa ni batili, walisema baada ya kusikiliza pande zote mbili, wameamua kuwa mkataba huo si batili na haujavunja sheria zozote za nchi.

“Mkataba wa IGA haukukiuka vifungu vya kikatiba na/au kisheria kama tulivyozinukuu hapo juu. Hoja za waleta maombi kwamba mkataba wa IGA ulipoka Uhuru wa Tanzania kumiliki na kutumia rasilimali asilia bila kuingiliwa hazikuwa na mashiko. Vilevile, Mahakama haijaona kama usalama wa nchi ulikuwa hatarini kutokana na kusainiwa kwa mkataba huo, ilisema sehemu ya hukumu hiyo.

Hukumu hiyo iliyosomwa jana katika Mahakama Kuu mkoani Mbeya, ilikuwa na takribani kurasa 91 na iliandaliwa na majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao ni Mustafa Ismail, Dunstan Ndunguru na Abdi Kagomba.

Walalamikaji katika kesi hiyo walikuwa ni Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus. Walioshitakiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge.

Katika kesi yao ya msingi waliyofungua, walalamikaji walikuwa na takribani hoja sita kuhusu suala hilo la IGA ya Tanzania na Dubai. Hoja hizo zilihusu; endapo utiaji saini, uwasilishaji na uridhiwaji wa IGA ulikiuka sheria, endapo umma ulijulishwa ipasavyo kuhusu suala hilo, endapo Katiba ya Tanzania – hasa ibara za 2,4, 6, 7, 8, 10 (1), 18, 21, 23 na endapo ibara za 26, 27 na 30 za IGA zinakiuka Katiba, endapo ibara za 2 na 23 za IGA zimekiuka kifungu cha 25 cha Sheria za Mikataba na endapo IGA ilifuata matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Tanzania.

Katika hukumu yao, majaji hao walipangua hoja moja baada ya nyingine miongoni mwa hizo zilizoletwa na waleta maombi na mwisho majaji hao wakaamua kwamba serikali haijavunja sheria yoyote wala Katiba katika uingiwaji wa mkataba huo uliovuta hisia za wengi.

Kwa mfano, majaji hao walisema kwamba hoja kwamba mkataba huo umekiuka Sheria ya Manunuzi haina mashiko kwa sababu hadi sasa – na kwa maana ya roho ya IGA hiyo, hakuna manunuzi ya aina yoyote yaliyofanyika na hivyo hakuwezekani kuwa na sheria iliyovunjwa.

Kuhusu hoja ya kuwa suala la mahakama za nje ya Tanzania kutumika katika kutatua migogoro itakayojitokeza ni kinyume cha sheria za nchi, majaji hao walisema suala hilo lina faida kwa pande zote mbili kwa sababu hakuna ajuaye ni lini mgogoro utatokea na utasababishwa na jambo gani na kifungu hicho kinalinda pande zote.

Katika eneo la endapo umma wa Watanzania ulijulishwa ipasavyo kuhusu IGA hiyo na kuwa uridhiwaji wake ulikiuka taratibu, Majaji hao walibainisha kwamba Bunge ni taasisi ambayo ni moja ya mihimili ya dola na kwamba taratibu na mipaka yake haviwezi kuingiliwa na taasisi au mihimili mingine.

Kuhusu suala la endapo kwamba mkataba huo unaingilia Uhuru wa Tanzania kuhusu umiliki wa ardhi yake na maliasili nyingine, majaji hao walihukumu kwamba hawajaona kitu katika IGA hiyo kinachoonyesha kwamba haki au Uhuru wa Tanzania na Watanzania utaathirika kwa chochote endapo DP World itaanza kazi zake kupitia mkataba huo.

“Kwenye suala la umiliki wa ardhi, hatujaona lolote kuonyesha kwamba uwekezaji huu utakiuka sheria za nchi au kupora ardhi ya Watanzania. Masuala ya umiliki wa ardhi nchini Tanzania yanasimamiwa kupitia sheria mbalimbali. Kwenye masuala ya uwekezaji, sheria inasema wazi kwamba ardhi itatolewa kupitia Kituo cha Uwekezaji ambao ndiyo watakuwa wamiliki wa ardhi hiyo.

“Suala kwamba Tanzania ikiingia mkataba na Dubai haitaruhusiwa kuzungumza na wawekezaji wengine pia halina mashiko. Kifungu hicho kimewekwa kwa lengo tu la kuhakikisha kuwa kubadilishana kwa taarifa miongoni mwa wabia hao wawili. Suala la kutoa taarifa kuhusu fursa za uwekezaji linafanywa kila siku kupitia balozi zetu zilizo katika nchi mbalimbali duniani na hakuna sheria yoyote inayovunjwa, ilisema sehemu ya hukumu hiyo.

Mmoja wa waliokuwa mawakili wa waliofungua kesi hiyo, Boniface Mwabukusi, aliwaambiwa waandishi wa habari kwamba wateja wake tayari wamemuarifu kuhusu dhamira yao ya kwenda kukata kukata rufaa kwenye Mahakama ya Rufani hapa nchini kuhusu suala hilo.

Mwisho

error: Content is protected !!