Mapato ya uwindaji wa kitalii yaporomoka

HomeKitaifa

Mapato ya uwindaji wa kitalii yaporomoka

Mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii unaofanyika katika mapori tengefu na mapori ya akiba Tanzania yameporomoka kwa Sh1.3 bilioni ndani ya mwaka mmoja.

Utalii huo huusisha uwindaji wa wanyamapori katika maeneo yaliyotengwa, upigaji picha na watalii kujionea wanyama hao.

Kwa mujibu hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka ujao wa fedha, mwaka huu wa 2021/22, Serikali imeingiza Sh23.6 bilioni kutokana na uwindaji wa kitalii kutoka Sh24.9 bilioni za mwaka 2020/21.

Huo ni sawa na upungufu wa Sh1.3 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Hata hivyo, mapato hayo yanaweza kuongeza kidogo kwa sababu mwaka wa fedha wa 2021/22 unaisha Juni 30.

Mapato ya uwindaji wa kitalii yamekuwa yakipanda na kushuka tangu mwaka 2017/18 kutokana na idadi ya watalii na wanyamapori wanaowindwa katika mapori yaliyoanishwa likiwemo Pori Tengufu la Loliondo mkoani Arusha.

Katika kipindi hicho cha miaka mitano iliyopita, mwaka 2017/18 ndiyo ulikuwa na mapato mengi yanayofikia Sh29.8 bilioni.

Pia wawindaji 2,250 waliendesha shughuli za uwindaji na Tanzania ilipokea watalii 1,770.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori (TAWA), shughuli za  Uwindaji wa kitalii hufanyika kwenye  mapori ya akiba, mapori tengefu,  maeneo ya usimamizi wa wanyamapori na vitalu vya uwindaji nje ya maeneo ya hifadhi.

Tanzania ina jumla ya mapori ya akiba 27, mapori tengefu (26), maeneo ya hifadhi za wanyamapori 21 ambapo  maeneo hayo yapo  chini ya uangalizi wa TAWA.

Mipango ya Serikali kuendeleza uwindaji wa kitalii

Kutokana na mapato ya Serikali yatokanayo na uwindaji wa kitalii kushuka, Serikali imekusudia kufanya maboresho mbalimbali ili kuendeleza uwindaji wa kitalii na kuongeza mapato ya Serikali kwa mwaka ujao.

Kupitia filamu ya “Tanzania The Royal Tour”, Serikali imejipanga kuendelea kutangaza maeneo ya uwekezaji katika sekta ya utalii.

“Sambamba na hilo Serikali  itaendelea kuhamasisha ufugaji wa wanyamapori ili watu, makampuni na mashirika binafsi waweze kuanzisha ranchi, bustani na mashamba ya wanyamapori,” alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana katika hotuba ya wizara yake kwa mwaka 2022/23.

Pia kitaanzishwa kitengo cha ukamataji wa wanyamapori kwa ajili ya mbegu ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama na ukarabati kiwanja cha ndege katika Pori la Akiba Moyowosi, Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, nyumba moja ya mtumishi Kunduchi na ujenzi wa vimbweta vinne katika Pori la Akiba Pande.

Huenda mipango hiyo ya Serikali ikasaidia kuongeza mapato wakati huu ambao mataifa mbalimbali yanaendelea kurejesha sekta ya utalii katika hali ya kawaida baada ya kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na Uviko-19.

error: Content is protected !!