Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango ametoa mapendekezo matatu yatayosaidia kuimarisha uwezo wa rasilimali watu barani Afrika ikiwemo taasisi za elimu kutoa mafunzo yenye suluhu za kukabiliana na changamoto za Afrika.
Kwa muda sasa wadau wa elimu, wamekuwa wakishauri kufanya maboresho ya mitaala ya elimu itakayowawezesha wahitimu kuajirika au kuwa na uwezo wa kujiajiri tofauti na sasa ambapo wahitimu wengi hutegemea zaidi kuajiriwa.
Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) vijana milioni 10 hadi 12 huingia katika soko la ajira kila mwaka huku vijana milioni tatu pekee wakifanikiwa kupata ajira.
Makamu wa Rais Dk.Mpango aliyekuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu jana Julai 25,2023 amewaambia washiriki kuwa taasisi za mafunzo na elimu zina mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya rasilimali watu.
Mpango ameongeza kuwa mchango wa taasisi hizo unapaswa kujielekeza katika kusaidia Afrika kusimamia na kunufaika na rasilimali asilia zinazopatika katika bara hilo.
“Afrika imekuwa ikitoa rasilimali fedha kwa ajili kukuza ujuzi ili kutumia katika kunufaika na rasilimali zetu, hivyo taasisi za mafunzo Afrika zinapaswa kushirikana ili kuja na suluhu mbalimbali kwa changamoto zinazoikumba Afrika”, amebainisha Dk. Mpango jijini Dar es Salaam.
Taasisi za fedha na sekta binafsi ziunge mkono
Mpango amesisitiza kuwa taasisi za fedha za kikanda na kimataifa zinapaswa kuja na mipango yenye ubunifu katika masuala ya fedha ili kusaidia ukuaji wa matumizi ya rasilimali watu katika bara la Afrika.
“Tunapaswa kufahamu kuwa matumizi ya rasilimali watu kwa uhalisia ni mpango wa muda mrefu na hivyo inahitaji taasisi za fedha za ndani ambazo zinatoa masharti nafuu”, amesema Dk Mpango.
Ili kuwakwamua vijana kiuchumi Tanzania imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zao, utaratibu ambao utaenda kubadilishwa kutokana na ubadhirifu pamoja na mikopo kutorejeshwa kwa wakati.
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, sekta binafsi inamchango mkubwa katika la ukuaji na matumizi ya rasilimali watu hasa wakishirikiana pamoja Serikali, hivyo mkutano huu utumike kama nyenzo ya kujadiliana njia bora ya sekta binafsi kushiriki kuimarisha rasilimali watu.