Matokeo zaidi ya 2,000 ya wanafunzi darasa la saba yafutwa, shule 24 zafungiwa

HomeKitaifa

Matokeo zaidi ya 2,000 ya wanafunzi darasa la saba yafutwa, shule 24 zafungiwa

Wakati maelfu ya watahiniwa wa mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2022 wakiwa na furaha baada ya matokeo yao kutangazwa, wenzao 2,194 wapo katika majonzi kutokana na hatua ya mamlaka ya usimamizi wa mitihani kufuta kabisa matokeo yao.

Kaimu Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Athumani Amas, aliyekuwa akitangaza matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2022, amewaambia wanahabari kuwa watahiniwa hao wamefutiwa matokeo yote kutokana na udanganyifu.

“Baraza la mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 2,194, sawa na asilimia 0.16 ya watahiniwa milioni 1.3, baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022, ” amesema Amas.

Idadi hiyo ya waliofutiwa matokeo ni mara tano zaidi ya watahiniwa 393 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2021.

Itakumbukwa Oktoba 25 mwaka huu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliagiza kufungwa kwa Shule ya Chalinze Modern Islamic Pre and Primary iliyoko mkoani Pwani  kuwa kituo cha mtihani kwa muda usiojulikana baada ya kubainika kufanya ufanganyifu kwenye mtihani wa darasa la saba.

Pamoja na kuyafuta matokeo ya watahiniwa hao Necta pia imezifungia shule 24  kuwa vituo vya mitihani ya Taifa baada ya kuthibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Shule hizo ambazo ni sawa na asilimia 0.13 ya vituo vyote vya mitihani nchini, ni pamoja na shule ya msingi Kadama iliyopo Chato- Geita, Rweikiza iliyopo (Bukoba), Shule ya msingi Kilimanjaro iliyopo (Arusha), Sahare  (Tanga), Ukerewe (Mwanza), Peaceland (Mwanza), Karume (Kagera), pamoja na Al-hikma ya  mkoani Dar es Salaam.

Shule nyingine ni Kazoba iliyopo mkoani Kagera, Mugini (Mwanza), Busara (Mwanza), Jamia (Kagera), Winners (Mwanza), Musabe (Mwanza), Elisabene (Songwe), High Challenge (Arusha), Tumaini (Mwanza), Olele (Mwanza), Mustlead (Pwani), Moregas (Mara), Leaders (Mara), Kivulini (Mwanza), St Severine (Kagera) na Shule ya Msingi St Anne Marie ya Dar es Salaam.

“Vituo hivi vimefungiwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha kanuni za mitihani mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya kitaifa,” amesema Amas.

Mkoa wa Mwanza ndiyo umeongoza kwa kuwa na vituo vingi vya mitihani vilivyofungiwa kwa kuwa na shule tisa, ukifuatiwa na jirani yake Kagera wenye shule tano, Mara (2), Arusha (2), Geita (1), Dar es Salaam (2), Pwani (1), Tanga (1) na mkoa wa Songwe ukiwa na shule moja.

error: Content is protected !!