Mawaziri wa Madini wa nchi za Afrika wamekubaliana kwa kauli moja kuweka mikakati ya kuongeza thamani ya madini katika nchi zao hususani madini ya kimkakati ili kuongeza mapato ya mataifa, kukuza uchumi na kuzalisha ajira katika nchi hizo.
Akizungumza kando ya Kongamano la Mining Indaba jijini Cape Town, Waziri wa Madini wa Tanzania, Anthony Mavunde amesema kuwa ametumia jukwaa hilo kutoa uzoefu wa Tanzania kuhusu namna Sekta za Nishati na Madini zinavyoshirikiana kwa vitendo katika kutekeleza ajenda ya uongezaji thamani wa madini kwa manufaa ya watanzania.
Waziri Mavunde ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika ili kuimarisha shughuli za madini ikiwemo kufikisha umeme wa uhakika katika maeneo ya uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani ya madini.
Mkutano wa Kimataifa wa ‘Mining Indaba 2026’ unaendelea jijini Cape Town, Afrika Kusini na unatarajia kukamilika Februari 12, 2026.
Tanzania inashiriki mkutano huo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kujiweka kama mshirika muhimu katika mnyororo wa kimataifa wa uzalishaji wa madini, hususan katika kipindi ambacho bara la Afrika linaendelea kutambuliwa kama mhimili muhimu wa uzalishaji wa madini yanayohitajika kwa ajili ya nishati safi na maendeleo ya viwanda duniani.


