Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akikaribia kumaliza rasmi ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani Morogoro, ametoa shukrani kwa wananchi kwa mapokezi mazuri waliyompatia.
“Ninawashukuru sana wananchi wote wa mkoa wa Morogoro kwa ukarimu na mapokezi mazuri kwa kipindi chote cha ziara yangu ya siku tano. Ninawashukuru pia kwa kujitokeza namna hii leo ninapohitimisha ziara yangu ndani ya mkoa huu,” alisema Rais Samia wakati akihutubia umati uliokusanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.
Rais Samia alieleza kuwa ziara yake mkoani Morogoro imekuwa na shughuli nyingi, akisisitiza kuwa viongozi wa mkoa walihakikisha kuwa amefanya kazi kwa bidii kubwa. “Ziara yangu ya kikazi imekuwa na kazi kweli kweli, Mheshimiwa mkuu wa mkoa na wenzie wamehakikisha wamenituma kweli kweli. Kwahiyo nimefanya kazi ndani ya mkoa huu kweli kweli,” aliongeza Rais.
Katika ziara hiyo, Rais Samia alijikita katika kukutana na kuzungumza na wananchi pamoja na kujionea maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia fedha za serikali.
Rais Samia pia alipata nafasi ya kujionea athari za mvua kubwa iliyonyesha katika mkoa huo, huku akifurahia juhudi zinazofanywa kurekebisha miundombinu iliyoathirika.
Kwa upande mwingine, Rais alifurahia mapokezi aliyoyapata na rekodi iliyovunjwa na wakazi wa Morogoro, hasa alipolala katika wilaya ya Kilombero kwenye mji wa Ifakara. “Nimefurahi katika ziara yangu hii, Morogoro mmevunja rekodi. Mmevunja rekodi kwa watu lakini mmeweza kunifanya nilale kwenye wilaya ya Kilombero pale kwenye wilaya ya Ifakara,” alieleza.
Pamoja na hayo, Rais Samia aliwahakikishia wananchi wa wilaya za Mlimba, Ulanga, na Morogoro vijijini kuwa atarejea kuwatembelea baada ya kuwa hakuwa na muda wa kutosha wa kuonana nao wakati wa ziara yake. “Naondoka Morogoro nikijua ndugu zangu wa wilaya za Mlimba, Ulanga, Morogoro vijijini bado sijawaona. Niliwaona kidogo pale Ngerengere, lakini ahadi yangu ni kwamba nitarudi tena kwa ajili yenu,” aliahidi Rais.
Ziara ya Rais Samia mkoani Morogoro imefanikiwa kwa kiwango kikubwa, na ameeleza kuridhika kwake kwa malengo yote ya ziara hiyo kutimia. “Ninafurahi pia kuwapa taarifa kwamba malengo ya ziara yangu yametimia,” alihitimisha Rais Samia.
Kesho, Rais Samia ataelekea Dodoma ambapo atatembelea kiwanda kimoja kabla ya kurejea rasmi makao makuu ya nchi.