Kamanda Mkuu wa Jeshi la polisi mkoani Dodoma, Onesmo Lyanga amethibitisha kuwa ni kweli Humphrey Polepole alivunjiwa dirisha la nyumba anayoishi na kuibiwa televisheni aina ya flat Screen inchi 55 na spika moja ya bluetooth huku thamani ya mali zote hizo ikiwa bado haijafahamika.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mbunge Humphrey Polepole alisafiri kwenda mkoa wa Manyara katika shughuli zake, upelelezi wenye kuambatana na msako mkali unaendelea ili kuwatafuta wahusika wa tukio hilo na kuwachukulia hatua za kisheria”. Alisema kamanda Lyanga.
“Suala la kwamba ni habari ya siasa sisi hatuoni kwasababu makazi yamevunjwa kwahiyo huwezi kusema wahalifu walikua wanamtafuta yeye, wangemkuta mwenyewe ishu ingekuwa tofauti ingekuwa ni unyang’anyi wa kutumia silaha au nguvu.
Bado haieleweki ni lini hasa palivunjwa kwa hiyo sio rahisi kujua kulikua na nia ya kutaka kumdhuru yeye kama yeye kwa sababu hakuna ujumbe wowote ambao tumeweza kuubaini kuwa umemtishia yeye maisha yake” aliongezea Kamanda Lyanga
Siku ya Jumapili ya Desemba 12 mwaka huu Humphrey Polepole aliweka video kwenye ukurasa wake wa Instagram ikionesha kuwa amekuta nyumbani kwake kumeibiwa na kuvurugwa, katika video hiyo vilionekana vitu vikiwa vimegazaa chini na yeye kusema kuwa anamuachia Mungu.