Ukitaka uzuri lazima udhurike

HomeMakala

Ukitaka uzuri lazima udhurike

Sio jambo la kushangaza katika miji mikubwa kama Dar es Salaam kuona vijana wakiwa wamebeba vikapu vyenye nyenzo za kutengenezea kucha na kuzunguka navyo wakitafuta wateja, ndani ya vikapu hivyo kuna rangi za kucha, brashi, msasa wa kusugulia kucha huku wakiwa wamening’iza taulo ndogo kwenye mabegani ili kuwahudumia wateja mitaani

Kwa vijana hao ni ajira kupaka watu rangi huku kwa wanawake ni urembo ili kuweza kupata muonekana mzuri wa kucha zao. Kucha hizo husuguliwa vizuri na kuoshwa na kisha kupakwa rangi kutokana na matakwa ya mteja au kubandika kucha za bandia (Tips).

Kwa sasa ni vijana wachache wanaozunguka mitaani wakitafuta wateja kwani wengi wamepiga hatua na kufungua sehemu zao maalumu za kazi ambapo wateja huwafuata na kupatiwa huduma hiyo mfano mzuri maeno ya Mwenge na Makumbusho ambapo ni maarufu kwa wapaka rangi kwani wanawake wanatoka sehemu mbalimbali na kwenda kwenye maeneo hayo kutengeneza kucha zao.

Baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakipata huduma hiyo, wameripoti kupata madhara ikiwemo kucha kuoza, kupata fangasi za kucha na wakati mwingine kucha zao kubadilika rangi. Siyo hayo tu, wengine huenda mbele zaidi na kuvimba vidole ikifuatiwa na majipu yanayotoa usaha na kucha kubanduka.

Hata hivyo, madhara hayo hutofautiana kati ya mtu na mtu kutegemeana muda na kiwango cha rangi alichopaka. Pia aina ya rangi na kukosea masharti ya upakaji kunaweza kuchangia hali hiyo.

“Ni takribani miaka 6 sasa tangu nimeanza kubandika kucha na kuzipaka rangi na nikiri kusema kwamba ukibandika kucha na kukaa nazo kwa muda mrefu basi lazima upate madhara, niliwahi kukaa na kucha kwa muda mrefu bila kuitoa mpaka kidole kikaanza kuuma na kutunga usaa , nilipokuja kutoa nilipata maumivu makali sana,” amesema Asmin Iddy mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.

Asmin pia alisema licha ya madhara hayo aliyoyapata lakini kwakubandika kucha kulimfanya awe anafanya shughuli zake polepole kwakuhofia kucha kukatika pia kwenye viatu unachagua sana na muda mwingine ukivaa lazima usikie maumivu. Mmliki mmoja wa saluni ya kike maeneo ya Mwenge Mpakani yeye ameiambia ClickHabari kwamba kidole chake kimoja kilioza kutokana na kubandika kucha za miguu bandia.

“Nina miaka miwili sasa tangu niache kubandika kucha zangu za miguu baada ya kidole changu kimoja kuoza kwa sababu yakubandika na kupaka sana rangi kwenye miguu kusema kweli kidole kiliuma sana,” amesema Diana.

Mwanafunzi mmoja wa chuo cha St Joseph’s Boko, Janeth Paul yeye pia amesema alikua akitoka Boko mpaka mwenge kwenda kubandika na kupaka rangi kucha lakini sasa ni takribani miezi 8 tangu aache kubandika kucha rangi.

“Kucha yangu moja ilioza miezi nane iliyopita na tangu hapo nimeacha kubandika kucha na kama nikipaka rangi basi sikai nayo sana naitoa kwani sitaki tena madhara haya yanitokee tena,” ameiamba ClickHabari Janeth.

Hata hivyo wapo wengine ambao wamesema hawajawahi kupata madhara yoyote yale yakiafya baada ya kubandika kucha wala kupaka rangi zaidi tu ya matatizo madogodogo.

“Mimi nabandika sana kucha na kupaka rangi kwa muda mrefu sana na sijawahi kupata madhara yoyote japo kuwa tu inabidi uwe makini pindi ubandikapo hasa wakati wakutandika kitanda kwan unaweza ukangoa kucha na pia wakutembea uwe makini usijigonge maana maumivu yake ni makubwa mno,” amesema Cypiana Kayombo.

Hellen Mpagama mkazi wa Sala Sala, Dar es Salaam yeye amesema kwamba amekuwa akibandika kwa muda mrefu na hajapata madhara yoyote isipokuwa anapata shida tu wakati wa kula na kushauri kwamba kama mtu asiwe anasugua sana kucha kwani kwakufanya hivyo unaweza kusugua mpaka kucha yako na kuiharibu.

“ sijawahi pata madhara yoyote yale ya kiafya kwa kubandika kucha na kupaka rangi, ispokuwa napata shida wakati wa kula hasa kama ni ugali, lakini pia nawashauri wasichana wenzangu kama mtu umeenda kutengeneza kucha hakikisha kucha hiyo haisuguliwi sana ikwani kwakufanya hivyo utaifanya kucha yako ibaki kama ilivyo kuliko kuisuguza sana,” amesema Hellen.

Aidha, unashauriwa kwamba endapo utabandika kucha hakikisha haukai nayo kwa muda mrefu kwani kwa kufanya hivyo unajiweka hatarini kupata madhara kama hayo yakuoza kucha, kukatika na kupata maumivu makali.

error: Content is protected !!