Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezitaka taasisi za Serikali au binafsi pamoja na mashirika kuacha urasimu katika utekelezaji wa miradi ya umeme, jambo litakaloongeza kasi ya kukamilika kwake na kuboresha maisha ya Watanzania.
Rais Samia aliyekuwa akishudia hafla ya utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa miradi mahsusi ya umeme jana Februari 14, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam amewaambia wahudhuriaji kuwa, urasimu ni miongoni mwa changamoto inayofanya miradi kutokamilika kwa wakati.
Kwa mujibu wa Rais Samia miongoni mwa mambo ambayo hukumbwa na urasimu katika utekelezaji wa miradi ya umeme ni pamoja na uchaguzi wa wakandarasi, utoaji wa vibali vya ajira, kutowajibishwa kwa watendaji wasio waaminifu pamoja na kucheleweshwa kwa malipo ya wakandarasi.
“Natambua kuna ambao walikuwa na wakandarasi wao mkononi na kwa sababu hakupata basi fitina nyingi, anazuia miradi isifanyike kwa matakwa yake binafsi, hatutakwenda hivyo, ili tupate maendeleo ya haraka tunahitaji maamuzi ya haraka, “ amesema Rais Samia.
Samia amezisisitiza mamlaka zinazohusika kutofumbia macho mambo yatayokwamisha utekelezaji wa miradi kwa wakati ikiwemo kesi na mashauri ambayo hufunguliwa na wakandarasi wanaokosa tenda.
Ajira zitoke kwa wakati
Rais Samia amekemea pia urasimu katika utoaji wa vibali vya ajira kwa wakandarasi kwa kuzitaka taasisi na mamlaka zinazohusika kutokuwa na mlolongo mrefu ambao unachelewesha utekelezaji wa mradi.
“Kama taasisi inataka wafanyakazi, mishahara ya kulipa wanayo, kwa mradi , kwa kazi fulani, wapewe ruhusa wafanye, ili miradi itekeleze kwa haraka, na kuzungushwa huku watu wanatafuta kupendeleana, tunadidimiza maendeleo,” amesema Rais Samia kwa msisitizo.
Miongoni mwa miradi iliyotiwa saini leo ni pamoja na mradi wa Ujazilizi 2B unaokusudia kupeleka umeme kwenye vitongoji 1,522, kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi, kilimo pamoja na vituo vya afya ambayo itagharimu Sh385 bilioni.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati Januari Makamba amesema kwa sasa umeme unaozalishwa bado hautoshi ingawa juhudi za Serikali kujinasua na jambo hilo zinaendelea.
“Tulipo kwenye umeme leo ndipo tulipokuwa kwenye barabara mwaka 1990, umeme hautoshi, miundombinu haitoshi lakini tunafarijika Rais umechukua maamuzi ya kishupavu kuwa shida ya umeme iishe, “ amesema Makamba.