TANZANIA na Finland wamekubaliana kuimarisha biashara baina yao.
Rais Samia Suluhu Hassan alisema hayo Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya kuzungumza na Rais wa Finland, Alexander Stubb aliyeko nchini kwa ziara ya kitaifa.
Rais Samia alisema katika mazungumzo yao wamekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na biashara na alitaja sekta tisa za ushirikiano.
Maeneo hayo ni elimu, biashara, nishati, utalii, uhusiano wa kimataifa, uwekezaji, uhawilishaji wa teknolojia, madini na uchumi wa buluu.
“Maeneo haya tumekubaliana kuendeleza kwa dhati uhusiano wetu kwenye maeneo hayo ambayo ni fursa kwetu na katika maeneo hayo tumeongeza maeneo mapya ambayo ni uchumi wa buluu na nishati,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema wamekubaliana kuongeza idadi ya watalii kutoka Finland wanaokuja Tanzania na akasema mwaka jana walikuja watalii zaidi ya 5,097 na mwaka huu hadi sasa wamekuja watalii zaidi ya 1,000.
Katika elimu alisema Finland ni mshirika wa masuala ya elimu nchini na katika kuimarisha uhusiano baina yao wamekubaliana kuongeza ushirika kwenye eneo la elimu ya ufundi stadi na kuongeza walimu uwezo.
Rais Samia alisema pia wamekubaliana kukuza ushirikiano kwenye Chuo cha Uongozi ambacho kinatumika kuandaa viongozi.
Katika Tehama alisema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye vituo atamizi na biashara changa za uchumi wa kidijiti.
Aidha, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye sekta ya madini kwa kuangalia maeneo ya fursa za ujenzi wa viwanda vya madini ili kuyaongezea thamani.
Katika sekta ya misitu, Rais Samia alisema wamekubaliana kuongeza ushirikiano na kuwa katika ziara hiyo leo, Rais Stubb atashiriki uzinduzi wa programu ya misitu inayofadhiliwa na taifa hilo.
“Lakini pia tumewaambia kuhusu ajenda yetu ya nishati safi na tumewashirikisha waone fursa na kusaidia eneo hilo,” alisema Rais Samia.
Wamekubaliana pia kuongeza ushirikiano katika eneo la Bunge kwa kuangalia maeneo ya uhusiano baina ya mabunge ya nchi hizo.
Katika sekta ya biashara, Rais Samia alisema Rais Stubb amekuja na wadau wa sekta binafsi waone fursa za biashara na uwekezaji.
Aidha, alisema wamekubaliana kuongeza uhusiano wao wa kimataifa na kusema Tanzania itaendelea kushirikiana na Finland na hata katika Umoja wa Mataifa kukabiliana na changamoto za dunia.
Rais Samia alimshukuru Rais Stubb kwa kuendelea kufanya kazi na Tanzania ikiwa ni nchi ya pili kati ya nchi mbili barani Afrika zinazofanya kazi na taifa hilo sasa.
“Tunaishukuru Finland kwa kuendelea kutuamini kuwa mbia wake na kuichagua Tanzania kama moja ya nchi mbili za Afrika wanazofanya kazi nao,” alisema.
Rais Stubb kesho anatarajiwa kuhutubia jukwaa la wafanyabiashara wa Tanzania na Finland linalotarajiwa kujadili fursa za kiuchumi na biashara baina ya nchi hizo mbili.