Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutekeleza ahadi zake kwa vitendo baada ya kuzindua Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo mkoani Morogoro. Kiwanda hiki kinachozalisha tani 200-250 za sukari kwa siku, kinatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza upungufu wa sukari nchini, huku pia kikitoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 5,000.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kuwekeza ndani ya nchi na kuingia kwenye miradi ya pamoja. “Sekta binafsi iwekeze ndani ya nchi, waingie kwenye miradi pamoja na serikali,” alisema.
Pia, aliwapongeza wale wote waliowezesha kutengeneza ajira kupitia kiwanda hicho na kuwatakia mafanikio mema katika kuendesha mradi huo kwa manufaa ya taifa. Rais Samia aliendelea kusisitiza dhamira yake ya kuendeleza miradi yote iliyozinduliwa na watangulizi wake, akionyesha kwamba uzinduzi wa kiwanda hiki ni uthibitisho wa ahadi hizo.