Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi dhamira ya Serikali ya kuendeleza mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo, akihutubia leo katika kilele cha Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, katika Uwanja wa Nanenane ambao sasa umetangazwa rasmi kuwa Uwanja wa Dkt. John Malecela.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi, wakulima, wataalamu wa kilimo na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, Rais Samia alieleza hatua mbalimbali ambazo Serikali yake inaendelea kuchukua ili kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa, chenye tija, na kinachoweza kutoa ajira pamoja na kuchangia kikamilifu katika Pato la Taifa.
Miongoni mwa hatua hizo ni mpango wa Serikali kushirikiana na sekta binafsi kuingiza matrekta makubwa 355 pamoja na matrekta madogo 401, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo na kupunguza utegemezi wa zana duni kwa wakulima.
Katika kukabiliana na changamoto za visumbufu vya mimea, Rais Samia alieleza kuwa Serikali imenunua ndege moja maalum pamoja na ndege nyuki 101, zitakazotumika kudhibiti na kuchunguza visumbufu hivyo kwa ufanisi zaidi. Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mazao ya wakulima hayapotei kabla ya mavuno kutokana na mashambulizi ya wadudu au magonjwa.
Aidha, Rais alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa zana za kilimo kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma za ugani kwa wakulima, kuimarisha vituo vya utafiti wa kilimo, na kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji.
Maadhimisho ya Nanenane mwaka huu yamebeba ujumbe wa mwelekeo mpya wa kilimo chenye tija na kibiashara, huku Serikali ikionyesha nia ya dhati ya kuijenga sekta hiyo kuwa mhimili wa maendeleo ya uchumi wa viwanda na ustawi wa wananchi.