Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa mataifa tajiri kuongeza ufadhili wa masharti nafuu kwa Afrika ili kusaidia kumaliza tatizo la njaa.
Akihutubia mkutano wa G20 uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil, Jumanne, Rais Samia aliwasihi viongozi wa mataifa hayo kutoa ufadhili wa haki na kufuta madeni ya nchi za Afrika na zinazoendelea, ili kuimarisha juhudi za kupambana na umasikini na njaa kali.
Alisema kuwa usalama wa chakula na kupunguza umasikini ni vipaumbele vya Tanzania na Afrika nzima katika kusukuma mbele agenda ya Umoja wa Kimataifa dhidi ya Njaa na Umasikini.
“Hili linaendana na dhamira ya Tanzania kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan Lengo namba 2 (Kumaliza Njaa ifikapo 2030). Ujumbe wa Tanzania pia utazingatia upatikanaji wa ufadhili wa masharti nafuu kwa Afrika,” alisema Rais Samia katika mkutano huo ulioshirikisha viongozi wa dunia wakiwemo Rais wa Marekani Joe Biden, Rais wa China Xi Jinping, na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.
Rais Samia alielezea mashaka kuhusu msimamo wa sasa wa mataifa ya G20 juu ya kufuta madeni kwa nchi zinazoendelea, akionya kuwa Afrika inakabiliwa na changamoto zinazochangiwa na migogoro, sera za kimataifa zinazoongeza ukosefu wa usalama wa chakula, pamoja na upatikanaji mdogo wa masoko na maendeleo ya kiteknolojia.
“Leo, tuko kwenye dunia yenye utajiri mkubwa, lakini Afrika bado inahangaika na viwango vya juu vya umasikini, njaa, maradhi, utapiamlo, na uzalishaji mdogo,” alisema Rais Samia.
Aliongeza kuwa asilimia 61.5 ya nguvu kazi ya Tanzania inajihusisha na kilimo, hatua ambayo imeongeza uzalishaji wa chakula kwa asilimia 128 na kupunguza viwango vya umasikini hadi asilimia 26.4 mwaka jana.