Rais Samia: Mabadiliko ya tabia ya nchi yanaathiri Watanzania 60%

HomeKitaifa

Rais Samia: Mabadiliko ya tabia ya nchi yanaathiri Watanzania 60%

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliojadili athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia na kusisitiza umuhimu wa kutopuuzia juhudi za kukabiliana na janga hilo.

“Tuko katika kipindi ambacho wakati tunapambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi bado tunataabika na changamoto kubwa ya sasa ambayo ni Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO – 19) ambayo imeangusha sana hali ya uchumi na kufuta mafanikio yaliyokwishafikiwa katika miongo kadhaa ya kujenga jamii zetu,” amesema Rais Samia.

Amesisitiza pia kuwa ingawa watu wengi wanachukulia kirahisi kupanda kwa hali ya joto kama moja ya athari za mabadiliko ya tabia nchi, bado hali ni ya kusikitisha kwa nchi kama Tanzania kwani hali hiyo husababisha ukame  ambao ni athari mbaya kwa sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo, uvuvi na misitu ambazo zinachangia 30% ya pato la Taifa na kuathiri takribani 60% ya wananchi.

Mkutano huo ambao ni mfululizo wa mikutano ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 26 wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) utakaofanyika Glasgow, Uskochi mnamo mwezi Novemba, 2021, umejadili hatua za upatikanaji fedha kwa ajili ya kugharamia ustahimilivu na upunguzaji wa athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Wakati huo huo, Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Comoro, Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Rebecca Nyandeng Garang. Viongozi hao wamezungumzia kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.

Rais Samia ameelekeza kufanyika haraka kwa mikutano ya tume za kudumu za ushirikiano baina ya mataifa hayo ili kuangalia namna ya kuboresha zaidi mahusiano.

Aidha, Rais Samia amefanya mazungumzo na Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na shirika hilo hususani katika kusaidia wakimbizi walioko nchini Tanzania.

Filippo Grandi ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kwa takribani

Miongo sita sasa ambapo pia amependekeza kuwepo na mkutano katika ngazi ya wataalam baina ya UNHCR, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuondoa changamoto katika kuwahudumia wakimbizi.

Rais Samia ameelekeza kikao hicho kufanyika mara moja ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.

error: Content is protected !!