Rais Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika ya umma kujitegemea ili kuongeza kipato kitakachopunguza mzigo wa utegemezi kwa Serikali na kukuza uchumi wa nchi.
Itakumbukwa alipokuwa akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali Machi 29, 2023 aliagiza kufanyika kwa tathmini katika mashirika ya Umma ili kubaini yale yasiyo na faida na ikiwezekana yafutwe.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa mashirika ya Umma leo Agosti 19, 2023 jijini Arusha, amesema mashirika hayo yakijitegemea yatapunguza mzigo kwa Serikali na kukuza uchumi wa nchi.
“Hapa kwetu imekuwa tofauti taasisi na mashirika yamekuwa mzigo kwa serikali, mara nyingi nimekuwa nikisema yanakula Serikalini lakini hayarudishi kitu,” amesema Rais Samia.
Katika kikao kazi hicho kilichohudhuriwa na viongozi wa Serikali, Wakurugenzi wa bodi za mashirika pamoja na wawakilishi wa taasisi, Rais Samia ameagiza mashirika hayo kuanza kuuza hisa kwa wananchi kwa kuwa azma ya kuanzishwa kwa mashirika hayo ni kumilikiwa na wananchi.
Hisa hizo zitayasaidia mashirika ya umma kumudu gharama za uendeshaji pamoja kukuza mitaji itakayowawezesha kuzalisha zaidi na kutoa gawio kwa Serikali.
Kwa mujibu wa Rais Samia ununuzi wa hisa hizo utawezesha taasisi na mashirika hayo kuchangia maendeleo ya shughuli mbalimbali nchini ikwemo ujenzi wa miundombinu, utoaji wa huduma na kuchangia katika bajeti kuu ya Serikali.
“Mashirika yakajitafakari na yale yanayoweza kurudi sokoni kwa wananchi na kuuza hisa zake ziuze hisa, wananchi wawe na ushiriki, najua yapo mashirika ya aina hiyo lakini mengi yaelekee huko,” amesema Rais Samia.
Ili kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo mapungufu ya kisheria yaliyopo katika ofisi ya hazina, ukosefu wa mitaji kwa wakati, na vikwazo katika taratibu za ununuzi wa umma Rais Samia Samia amesema Serikali iko mbioni kutatua changamoto hizo ili mashirika hayo yazalishe zaidi.
“Tunaangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa mfuko wa uwekezaji wa umma ili kuondoa utegemezi kutoka mfuko mkuu wa serikali …sasa tunatoa yote hayo ili mashirika yakazalishe,”amesema Rais Samia.
Ahueni nyingine zilizotangazwa katika ufunguzi wa kikao hicho ni Mabadiliko ya sheria ya ununuzi wa umma, uhuru wa taasisi kujiendesha katika mambo ya msingi na maboresho katika utoaji wa ajira za taasisi.