Rais Samia: Tutafungua mikono kwa wote watakaotuunga mkono

HomeKitaifa

Rais Samia: Tutafungua mikono kwa wote watakaotuunga mkono

Rais Samia Suluhu Hassan amehimiza ushirikiano wa kimataifa kukabili changamoto likiwemo janga la UVIKO-19, uchumi na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Rais Samia amesema hayo jijini New York, Marekani wakati akihutubia Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba anatambua na anaamini katika ushirikiano katika kutatua changamoto zinazoikabili dunia.

“Tutafungua mikono yetu kwa wale wote watakaotuunga mkono na tutaendelea kuwa nchi ambayo inategemewa na mataifa mengine. Tanzania, nchi ambayo kwa heshima imekuwa ikishirikiana na nchi nyingine bila kujali kama ni nchi kubwa au ndogo, tajiri au masikini, imara au dhaifu,” amesema.

Ameongeza kuwa UVIKO-19s umeonesha dunia umuhimu wa nchi kushirikiana na madhara ya kujitenga bila kujali ukubwa au eneo kijiografia. Amesema wakati dunia inakabili changamoto za korona, imebaki miaka isiyozidi 10 kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Rais Samia amesema kwa mujibu wa ripoti ya tathimini iliyofanywa kuhusu utekelezwaji wa malengo hayo, kwa sasa dunia iko nyuma katika kufikia malengo hayo na sababu kubwa ni athari za virusi vya korona.

Aidha, amehimiza nchi zinazoendelea zisaidiwe kukabili athari zilizotokana na ugonjwa wa UVIKO -19 na amepongeza mashirika ya fedha ya kimataifa kwa jitihada za kuokoa uchumi wa nchi nyingi usianguke kutokana na janga hilo.

“Hatua zilizotangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zilichukuliwa ikiwemo Tanzania kujiunga na COVAX ili kuhakikisha watanzania nao wanapata fursa ya kuchanjwa dhidi ya Korona,” amesema.

error: Content is protected !!