Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imetoa wito kwa wananchi wa Namibia kukumbatia amani na umoja kabla, wakati na baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumatano Nov 27.
Mwenyekiti wa Asasi hiyo na Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka wahusika wote wa kisiasa nchini Namibia na wafuasi wao kuhakikisha wanachukua hatua stahiki ili siku ya uchaguzi iwe yenye mafanikio, utulivu, amani na hata baada ya uchaguzi.
Rais Samia alisema kwa kuzingatia marekebisho ya Kanuni na Miongozo ya SADC ya Kusimamia Uchaguzi wa Kidemokrasia (2021), ambayo ilipitishwa na Nchi Wanachama wake, SADC imetuma Ujumbe wake wa Waangalizi wa Uchaguzi (SEOM) nchini Namibia kuangalia awamu ya kabla ya uchaguzi wa nchi hiyo. Ujumbe huo pia utashiriki uangalizi siku ya uchaguzi na taratibu za baada ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa Rais Samia, lengo ni kuhakikisha Namibia inazingatia masharti husika ya Kanuni na Miongozo ya SADC.
“Kanuni na Miongozo hii inakuza chaguzi za mara kwa mara, huru, za haki, za uwazi, za kuaminika na za amani kama alama kuu za demokrasia na utawala bora katika ukanda wa Kusini mwa Afrika,” alisema.
Aliongeza; “Kama kanda, tunatarajia michakato ya uchaguzi inayozingatia maadili na kanuni za kidemokrasia zilizoainishwa katika Mkataba wetu wa SADC, Itifaki ya SADC ya Siasa, Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama, na Kanuni na Miongozo ya SADC inayoongoza Uchaguzi wa Kidemokrasia (2021).