Serikali kubadili umri wa mtoto wa kike kuolewa

HomeKitaifa

Serikali kubadili umri wa mtoto wa kike kuolewa

Serikali inakusudia kufanya mabadiliko ya Sheria ya Ndoa ya Tanzania ambayo kwa muda mrefu sasa imekuwa moja sheria ambazo zinakumbana na upinzani mara kwa mara, hadi kupelekea kesi kufunguliwa mahakamani.

Hilo limesemwa bungeni na Wizara ya Katiba na Sheria ikitoa majibu ya swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Katimba ambaye aliitaka serikali ieleze ni lini itapeleka musawada wa Sheria ya Ndoa ili kurekebisha vifungu vyenye mapungufu hususani kifungu kinachohalalisha mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri chini ya miaka 18.

Wizara ya Katiba na Sheria imeeleza kwamba muswada huo umeshafikishwa kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria tangu Februari 2021 na kwamba utafikishwa bungeni baada ya kukamilisha michakato mbalimbali ikiwemo kushirikisha wadau wengi kutoa maoni yao.

Wizara imeeleza kwamba Muswada huo ulifikishwa kwa kamati hiyo kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Rufani katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebecca Gyumi, rufani namba 204/2017 na namba 5/2016 ya Mahakama Kuu iliyotaka Sheria ya Ndoa ifanyiwe marekebisho ili mtoto wa kike aolewe akiwa na miaka 18.

Wizara ilifanya mapitio ya sheria hiyo na kuona uhitaji wa kushirikisha wadau ili kupata maoni zaidi, baada ya kupata maoni na kukamilika kwa taratibu zote muswada huo utafikishwa bungeni.

error: Content is protected !!