Rais Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na mabadiliko ya kiuchumi duniani, Serikali itafanya mapitio ya Sera yake ya mambo ya nje iliyodumu kwa miaka 20.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 19, 2022 wakati wa mkutano wake na Mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya Nchi, unaofanyika Zanzibar ikiwa ni mara ya kwanza kukutana na mabalozi hao 61 tangu alipoingia madarakani Machi, 2021.
Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa lengo la kuakisi mazingira na mahitaji mapya ya kidunia katika diplomasia.
“Hali ya uchumi wa dunia imebadilika katika muongo mmoja, Sera yetu ya mambo ya nje ina miaka 20, tunayoitumia sasa hivi, mkutano wetu wa mwisho wa mabalozi ulikuwa mwaka 2019, “amesema Rais Samia akifafanua:
“Kwa hiyo kuna mambo mengi yamebadilika ndani ya dunia kwa hiyo nasi ni sahihi tuangalie sera yetu yenye miaka 20, je bado ina mashiko katika mabadiliko ya dunia kwa sasa hivi, lakini je ndani miaka minne kuna mambo gani yametupita.”
Rais Samia amesema katika kipindi chake dhamira imekuwa ni kuongeza uhai wa diplomasia ya Tanzania kupitia damu mpya ya vijana katika nafasi za mabalozi, kupanua balozi mpya, kushiriki mikutano ya kimataifa na ziara za kimkakati zinazofungua fursa za kiuchumi na mashirikano.