Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewarejesha salama nchini Watanzania 42 waliokuwa wakiishi Israel na Iran kufuatia mvutano wa kijeshi unaoendelea kati ya mataifa hayo.
Akizungumza katika mapokezi ya Watanzania hao Juni 25, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha usalama wa raia wa Tanzania waliokuwa maeneo ya hatari.
“Serikali imegharimia gharama zote kuhakikisha Watanzania wetu wanarejea salama. Kundi lingine kutoka Iran linatarajiwa kuwasili kesho,” alisema Dkt. Shelukindo.
Aidha, alitoa wito kwa Watanzania kuendeleza utulivu na amani ndani ya nchi, akisisitiza kuwa hayo ndiyo msingi wa usalama wa Taifa.
Mmoja wa wanafunzi waliorejea kutoka Israel, Bi. Neema Dasina, alieleza kuwa hali ya usalama ilikuwa mbaya lakini serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na balozi zake Israel na Misri, ilihakikisha wako salama hadi kurejea nyumbani.
Kwa upande wake, Bi. Asela Luena, mama wa mmoja wa vijana waliorejea, ameishukuru serikali kwa juhudi za dhati za kuwaokoa watoto wao na kurudisha furaha ndani ya familia zao.