Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekusanya zaidi ya Sh bilioni 86.31 katika siku ya kwanza ya kampeni yake ya kuchangishana inayolenga kukusanya Sh bilioni 100.
Kati ya pesa zilizokusanywa kiasi cha Sh bilioni 56.3 zilikuwa ni fedha taslimu na zaidi ya Sh bilioni 30.02 zikiwa ni ahadi za michango. Michango hiyo imetokana na wananchi, wanachama na wapenzi wa chama wakijitokeza kuunga mkono shughuli za kampeni na ujenzi wa Makao Makuu mapya ya chama hicho.
Miongoni mwa wachangiaji wakubwa ni wachimbaji wadogo waliotoa Sh bilioni 16, wafanyabiashara wa Kariakoo waliotoa Sh milioni 500, wageni mashuhuri walioketi meza kuu walichangia jumla ya Sh milioni 270, wakiwemo Dk. Philip Mpango (Sh milioni 20), Dk. Hussein Mwinyi (Sh milioni 50), Kassim Majaliwa (Sh milioni 20), Hemedi Suleiman Abdallah (Sh milioni 20), Stephen Wasira (Sh milioni 20), Dk. Tulia Ackson (Sh milioni 20) na Zuber Ally Maulid (Sh milioni 20).
CCM upande wa Zanzibar ilichangia Sh bilioni 4 na kuahidi Sh bilioni 1 zaidi. Kampuni ya GSM, kupitia Rais wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said, ilitoa Sh bilioni 10, huku Klabu ya Yanga ikiahidi Sh milioni 100. Mawaziri na Naibu Mawaziri wamechangia Sh milioni 365 pamoja na makundi na taasisi mbalimbali kutoka sehemu tofauti nchini.