1. Malengo ya kusaidia wengine
“Kama unaanzisha biashara kwa malengo ya kuwa tajiri, hakika hutokua”.. John D. Rockefeller. Facebook ilipoanzishwa na Mark Zuckerberg, haikuwa na lengo la kupata fedha, bali lengo lake ni kuwafanya wanafunzi wa Chuo cha Havard kuweka picha na taarifa zao kwa mawasiliano tu. Hivyo basi, matajiri wengi wakubwa huanzisha miradi mbalimbali ikiwa na lengo la kurahisisha maisha ya watu, kuwafanya watu wawe na furaha na kuwasaidia kutimiza malengo yao. Baada ya muda, unaweza sasa kufikiria kupata fedha kwenye jitihada zako huku ukiendelea kuwa msaada mkubwa kwa watu.
2. Kusoma Vitabu
Bill Gates wa Microsoft, Oprah Winfrey, Elon Musk na Warren Buffet wana ukwasi wa hali ya juu, na jambo moja walilokuwa nalo ni kupenda sana kusoma vitabu. Tabia hii sio kama wameanza baada ya kupata fedha, bali ni tabia waliyokuwa nayo muda mrefu. Bill Gates husoma vitabu 50 kila mwaka, wastani wa vitabu vinne na nusu kila mwezi. Warren Buffet hutumia 80% ya siku yake kusoma vitabu.
3. Kuwa na mikakati ya fedha ya muda mrefu
Matajiri wengi hutegemea mipango ya muda mrefu kuanza kuvuna fedha kwenye miradi yao, na sio ya muda mfupi. Matajiri hawawekezi pesa zao kwenye mambo wasiyo na ujuzi nayo wa kutosha, lazima wafanye tafiti na wajifunze zaidi kuhusu kitu hicho, kujua faida na hatari zake na namna ya kuziepuka, kisha wanawekeza hela kwa malengo ya muda mrefu.
4. Hakuna kukata tamaa
Mafanikio hubeba historia za mateso na maumivu makubwa. Matajiri wengi wamepitia mateso na maumivu makubwa katika harakati zao za kutafuta pesa. Kama wangalikata tamaa mapema, pengine wasingalikuwa na utajiri walionao leo. Mfano mzuri ni Colonel Harland Sanders mwanzilishi wa Kampuni ya KFC, kuku wake na fomula ya ladha yake ilikataliwa mara 1,009 kabla ya kukubaliwa, lakini sasa hivi migahawa ya bishara yake iko takribani dunia nzima.
5. Kubali kukosolewa
Kukubali kukosolewa ni moja ya tabia za matajiri wakubwa. Hawachukii kukosolewa, bali huchukua matamko ya watu wanaowakosoa na kuyafanyia kazi. Tajiri namba moja duniani, mwanzilishi wa kampuni ya Amazon anasema, “Wale wenye ndoto za kuanzisha vitu vipya, basi wawe tayari kukosolewa”.