Katika medani ya kimataifa, kila Taifa duniani lina namna yake ya kushirikiana na mataifa mengine katika kuhakikisha kuwa Taifa linapata maslahi yake. Mipango na mikakati ya Taifa katika kupigania maslahi yake huundwa kwa Sera za Mambo ya Nje (Foreign Policy).
Dira ya Taifa katika medani ya kimataifa inaweza kuamuliwa na Bunge la Taifa husika, au hata Rais aliyekuwa madarakani, anaweza kuamua dira ya Taifa kutokana na matendo na mienendo yake. Mathalan, Hayati Nyerere alijibainisha kimkakati kupitia Azimio la Arusha, sera ya kutofungamana na upande wowote wakati wa Vita Baridi na ukombozi wa nchi za kusini mwa Bara la Afrika.
Vivyo Hivyo Rais Mwinyi akajibainisha na mpango wake Ruksa, kufungua masoko kwa bidhaa za nje na mashirika binafsi kuanza kuhodhi mali za serikali kupitia sera ya ubinafsishaji. Hayati Mkapa na Hata Rais Mstaafu Kikwete mpaka Magufuli, hawa wote utagundua kuwa kila mmoja alikuwa na namna yake ambayo iliakisi dira ya Taifa kulingana na maslahi ya Taifa.
Utaratibu huu upo takribani dunia nzima, ikiwa lengo la kila kiongozi ni kuona kuwa Taifa linapata matunda na kila Mwananchi ananufaika. Mfano Rais aliyepia wa Marekani alizifungia takribani nchi 7 za kiislamu kutokuingia Marekani akiwa na lengo la kuimarisha amani nchini Marekani, lakini Biden alipoingia tu madarakani akaondoa zuio hilo la mtangulizi wake, hatua hizi mbili za marais wa Marekani ziliamua aina ya mahusiano na nchi husika na pia mataifa mengine, aidha kuwa mabaya au mazuri.
Sera za Mambo ya Nje hubadilika kulingana na wakati na mabadiliko ya Dunia. Matukio kama ya Ugaidi, mabadiliko ya tabia nchil na hata masuala ya silaha za maangamizi kama vile nuklia yanaweza kuamua mahusiano ya Serikali moja na nyingine, na kila moja kutafuta namna ambayo inaweza kulinda maslahi yake.
> Jumuiya ya Africa Mashariki yaunga mkono kauli ya Rais Samia Umoja wa Maifa
Ikiwa lengo ni kutimiza maslahi mapana ya Taifa, basi ipo namna ambayo Rais Samia anajibainisha mbele ya mataifa mengine katika kuileta Tanzania maendeleo chanya. Tangu Rais Samia aingie Madarakani 19 Machi 2021 zipo hatua kadhaa amezichukua ambazo zinabainisha dira ya maendeleo ya Tanzania kwa sasa katika medani ya kimataifa, ambapo anarudia yaleyale ya watangulizi wake katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata maendeleo chanya. Licha ya kwamba utaratibu wake unaweza kuwa tofauti na wengine, lakini dhamira ya viongozi wote hawa ni mafanikio kwa Taifa la Tanzania.
Mienendo ya Rais Samia inaonesha dhahiri kuwa yeye ni muumini mkubwa wa Sera za Kiliberari. Kwani punde tu alipoingia madarakani kwenye moja ya hotuba zake ni kuondoa adhabu dhidi ya vyombo vyote vya habari nchini Tanzania. Hatua hii ilifanya apongezwe na mataifa mengi makubwa duniani.
Pili Rais Samia alianza kuonekana kupunguza masharti katika uwekezaji Tanzania, kampuni za uchimbaji wa madini, gesi na sekta mbalimbali walianza kumiminika nchini kutafuta fursa za uwekezaji. Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inaonesha kuwa Tanzania katika kipindi cha miezi matatu (Machi – Agost 2021) uwekezaji umekuwa mara sita zaidi ya kipindi kama hicho mwaka 2020 wakati wa Hayati Magufuli, hii ni dalili moja wapo kuoenesha namna gani Rais Samia anacheza karata zake katika medani ya kimataifa.
Rais Samia kuhudhuria kwake na kuhutubia katika Mkutano Mkuu wa 76 wa Umoja wa Mataifa, ni moja ya ishara kubwa pia Rais Samia anataka kuboresha urafiki na ushirikiano na mataifa makubwa duniani. Hatua hii inaweza kukaribisha uwekezaji Tanzania na hata uchumi kukua zaidi. Kila siku zinavyosonga mbele Rais Samia anazidi kujenga marafiki wengi na kupunguza maadui. Wakati wa Magufuli aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Prof. Palamagamba kabudi kwenye moja ya Mkutano huo.
Hatua ya Rais Samia kuruhusu chanjo nchini imepewa heko nyingi sana na mashirika ya kimataifa pamoja na mataifa makubwa. Hatua hii imeboresha na kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na mataifa mengine. Hii ni namna ambayo Rais Samia anaitumia katika kujibainisha yeye ni mtu wa aina gani katika kuitambulisha Tanzania kwenye medani ya kimataifa.
Leo tarehe 30 Septemba 2021 Rais Samia amesafiri kuelekea Glasgow nchini Scotland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kujadili masuala mabadiliko ya tabia nchi (COP26). Tafsiri yake ni kwamba Rais Samia bado anafanya yaleyale ya watangulizi wake katika kuimarisha uchumi wa Taifa la Tanzania. Rais Samia anakwenda kutengeneza fursa za uwekezaji, anakwenda kutengeneza marafiki na kuitangaza Tanzania katika namna yenye manufaa.