Tanzania ina umeme wa kutosha

HomeKitaifa

Tanzania ina umeme wa kutosha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchemsi Mramba, amesema Tanzania ina umeme wa kutosha kwa matumizi yake na kuuza nchi zingine, huku akitaja faida za kunua umeme Ethiopia kwa matumizi ya Kanda ya Kaskazini.

Hali ya uzalishaji umeme nchini hivi sasa ni nzuri. Tanzania inazalisha megawati 3,796 huku mahitaji yakiwa megawati 2,200 na ziada hiyo inatarajiwa kuuzwa nje ya nchi.

Mramba alisema umeme huo unazalishwa katika vyanzo mbalimbali vilivyopo mikoa ya Kusini, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara na Pwani, hususan Bwawa la Julius Nyerere.

“Umeme huu kwa asilimia kubwa unazalishwa Nyanda za Kusini, hivyo unapotoka kusafirishwa maeneo mengine hususan Nyanda za Kaskazini zinatumika gharama kubwa na kusababisha upotevu mkubwa wa megawati na kusababisha hasara,” alisema.

Kwa mujibu wa Mramba, megawati 17 zinapotea ikiwa ni hasara kubwa kwa Taifa kwa kuwa nishati hiyo inaweza kutosha Mkoa wa Songwe unaotumia megawati 14.

Changamoto ya umeme unaofika Nyanda za Kaskazini ikiwemo Arushaa unakuwa dhaifu kwa sababu ya kuwa na msongo wa umeme mdogo, hali inayotokana na usafirishaji mrefu kutoka Nyanda za Kusini katika vyanzo vya uzalishaji, hivyo umeme unapotea kwa wingi.

Usafirishaji Umeme

Mramba alifafanua kuhusu umbali wa usafirishaji umeme kutoka Ethiopia kufika nchini ni kwamba umeme huo hauchukuliwa moja kwa moja Ethiopia, bali nchi hiyo inaingiza Kenya na Tanzania inauchukua Kenya kupitia mpaka wa Namanga hivyo mita zinafungwa mpaka kwa mpaka.

“Gharama za umeme hu oni ndogo ambapo n idola za Marekani senti 7.77 ikilinganishwa na dola senti 10 za usafirishaji wa umeme wa ndani kutoka Kanda ya Kusini. Hivyo ni faida zaidi kununua kutoka Ethiopia kwani hausafirishwi kwa umbali mrefu kutokea Kenya,” alisema.

error: Content is protected !!