TPDC yasaini mikataba ya Sh60 bilioni kuongeza umiliki wa kitalu

HomeKitaifa

TPDC yasaini mikataba ya Sh60 bilioni kuongeza umiliki wa kitalu

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeongeza mara mbili umiliki wa kitalu cha gesi asilia cha Mnazi Bay baada ya kusaini mikataba miwili ya mauziano na uendeshaji na kampuni ya nishati ya Ufaransa, Maurel & Prom, hatua itayoongeza nguvu katika uendelezaji na uendeshaji wa mali hiyo muhimu katika uzalishaji wa nishati nchini.

Mikataba hiyo iliyosainiwa leo (Februari 3, 2024), Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, ni matokeo ya majadiliano baina ya pande zote mbili baada ya Maurel & Prom kununua hisa za mbia mwingine Wentworth Resources aliyekuwa ana miliki asilimia 31.94 katika mradi huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame amesema shirika hilo sasa litakuwa linamiliki kitalu hicho kwa asilimia 40 baada ya kununua asilimia 20 ya hisa kati ya asilimia 31.94 zilizokuwa zinamilikiwa awali na kampuni ya Marekani ya Wentworth Resources.

Kabla ya makubaliano ya leo kitalu cha gesi asilia cha Mnazi Bay kilikuwa kinamilikiwa na Maurel & Prom kwa asilimia 48.06, Wentworth (asilimia 31.94) na TPDC iliyokuwa inamiliki kwa asilimia 20.

Makame amesema awali Maurel & Prom ilikuwa imeingia makubaliano ya kununua hisa zote za Wentworth Resources katika kitalu hicho kilichopo mkoani Mtwara, uamuzi ambao ungeifanya kampuni hiyo ya Ufaransa kuwa na umiliki wa asilimia 80.

Hata hivyo, Makame amesema TPDC ilitumia sheria ya petroli inayoipa haki ya kwanza (first right of refusal) kununua hisa za mbia yeyote aliyemuua kuziuza na kuamua kununua asilimia 20 ya hizo zilizokuwa zinamilikiwa na Wentworth.

“Uamuzi wa kununua hisa hizo utasaidia kuongeza mapato kwa Serikali, kuimarisha usalama wa nishati nchini kwa kuepuka sehemu kubwa ya kitalu kumilikiwa na kuendeshwa na kampuni moja tena yenye asili ya nje ya nchi,” amesema Makame.

Zaidi ya Sh60 bilioni zatumika kukamilisha ununuzi huo

Katika makubaliano hayo, TPDC imeilipa Maurel & Prom Dola za Marekani milioni 23.6 sawa na Sh60 bilioni zenye thamani sawa na asilimia 20 ya hisa hizo zilizokuwa zinamilikiwa na Wentworth Resources katika kitalu hicho. Maurel & Prom tayari ilishakuwa imefanya makubaliano ya manunuzi ya hisa hizo za Wentworth Resources.

Kwa sasa, Makame amesema TPDC itakuwa na nguvu ya kufanya maamuzi katika uendelezaji na uendeshaji wa kitalu hicho ikiwemo kuwapeleka wafanyakazi wake kushiriki katika uendeshaji kwa muda mrefu.

Kitalu cha Mnazi Bay, kwa mujibu wa TPDC, kwa sasa kinakadiriwa kuwa na hifadhi ya gesi asilia inayoweza kuzalishwa (Recoverable natural gas reserves) ya futi za ujazo bilioni 641 na kila siku mradi unazalisha futi za ujazo zipatazo milioni 120 zinazosambwa kwa mteja wao mkubwa ambaye ni Tanesco.

Mkurugenzi Mkuu wa Maurel & Prom Tanzania, Nicholaus Engel amesema katika hafla hiyo kuwa uongezaji huo wa hisa unamaanisha kuwa kutakuwa na kiwango kikubwa cha kuzingatia rasilimali hiyo katika uendelezaji na upanuzi wa uzalishaji ili kumudu mahitaji ya sasa na baadaye ya nishati hiyo.

Maurel & Prom inamilikiwa kwa sehemu kubwa (asilimia 71.09) na kampuni ya mafuta ya Indonesia Pertamina Internasional EP (PIEP) huku Rais Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa uongezaji wa umiliki wa TPDC katika kitalu hicho ulikuwa ni sehemu ya mazungumzo yake na ya hivi karibuni na Rais wa Indonesia Joko Widodo.

Zaidi ya asilimia 60 ya umeme wa Tanzania unazalishwa kwa kutumia gesi asilimia huku takriban nusu au asilimia 48 ya gesi yote inayotumika ikizalishwa Mnazi Bay.

error: Content is protected !!