Mamlaka ya uteuzi imeongeza muda wa siku 42 kuanzia tarehe 20 Februari kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ili kukamilisha uchunguzi wake na kuwasilisha taarifa kabla au ifikapo Aprili 3,2026.
Awali, kwa mujibu wa Mpango Kazi, Tume ilipaswa kuwasilisha taarifa hiyo ifikapo Februari 20, 2026 ndani ya siku 90 tangu ilipoanza kutekeleza majukumu yake Novemba 20, 2025, mara baada ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Gazeti la Serikali la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muda huo umeongezwa ili kutoa fursa ya kutosha kwa kila mwenye taarifa, ushahidi au maoni, aliyepo ndani na nje ya nchi, kuwasiliana na Tume na kuhakikisha hakuna mtu au taasisi itakayokosa kusikilizwa.


