Rais Samia Suluhu Hassan Ameandika Historia Mpya ya Maendeleo, tumuunge mkono
Na GULATONE MASIGA
Tanzania imethibitisha kwamba inapoongozwa kwa utulivu, busara na dira sahihi ya maendeleo haiwezi kushindwa. Tulianza kwa hofu na mashaka, wengine wakamkatia tamaa Rais Dkt Samia Samia Suluhu Hassan aliposhika kijiti cha urais kufuatia kufariki kwa Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Leo tunashuhudia historia mpya ikiandikwa. Ni kweli kabisa, Tanzania imerudi kwenye meza ya dunia ikiwa na nguvu, heshima, kasi ya maendeleo na matumaini mapya kwa kizazi cha sasa na kijacho.
1. UMEME WA UHAKIKA KWA UCHUMI IMARA!
Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP – Mto Rufiji) limekamilika baada ya kukuta mradi ukiwa asilimia 30 tu. Leo umeingiza megawati 2,115 kwenye gridi ya taifa! Kwa pamoja na miradi ya uzalishaji wa umeme wa gesi mitambo ya Kinyerezi na Ubungo, Tanzania sasa inazalisha megawati 4,030 kwa mwaka kutoka Megawati 1,600 hapo kabla. Mpango wa sasa ni kuzalisha megawati 8000 ifikapo 2030.
Hii ni nguvu ya ajira, viwanda, uwekezaji, biashara, mitaji na ubunifu wa vijana. Kila kijiji kinaweza kuwa kiwanda na wananchi watumie umeme kujiajiri. Huku ndiko kujenga uchumi imara. Taifa linapiga hatua!
2. SGR KWA SAFARI ZA HARAKA NA GHARAMA NAFUU
Reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma imekamilika, treni zimeanza kutoa huduma. Kwa sasa muda wa safari kati ya Dar – Dodoma umepungua sana kutoka safari ya masaa 9 hadi masaa 4 tu na gharama za usafirishaji wa mizigo zimepungua kwa asilimia 40.
Vipande vipya kuzunguka kutoka Dodoma, Makutopora (Singida), Tabora, Isaka, Mwanza, Kigoma vinaendelea hadi Burundi na DRC.
Tanzania inageuka kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki. Nchi yetu inafunguka kama mlango wa fursa za kiuchumi kwa maelfu ya vijana na wafanyabiashara. Kesho yetu ni njema.
3. HUDUMA ZA AFYA ZIMEIMARISHWA NA ZIMESOGEA KARIBU NA WANANCHI
Kila hospitali ya rufaa ya mkoa na Kanda imewekewa CT Scan na MRI. Hii imepelekea kwa sasa hakuna tena safari ndefu kusaka vipimo.
Ujenzi wa Zahanati na vituo vya afya, ununuzi na usambazaji wa dawa, vitendanishi, vifaa na vifaa tiba, magari ya kubeba wagonjwa (Ambulance) pamoja na wataalamu na wahudumu wa afya kumeimarisha upatikanaji wa huduma ya afya katika ngazi ya msingi ikiwemo afya ya uzazi, tmama na mtoto.
Huu ndio uhai wa taifa, afya kwanza, maendeleo yanakuja bila hofu!
4. MAGEUZI MITAALA ELIMU – MTOTO AKIMALIZA KIDATO CHA NNE ANA UJUZI WA FANI
Kufuatia mtaala mpya ambao utaanza mwaka 2026/27 elimu yetu sasa inatoka kwenye nadharia kwenda kuwa elimu yenye kutoa maarifa ujuzi. Lengo likiwa ni kuwawezesha wahitimu kupata ujuzi wa fani yeyote ili waweze kukabiliana na changamoto ya ajira sokoni.
Kwa mtaala mpya mwanafunzi anayemaliza kidato cha 4 atapata vyeti viwili: cha elimu ya sekondari na VETA ambapo ataweza kujiajiri au kuajiriwa popote
Tumeshuhudia pia ujenzi wa vyuo vipya vya VETA katika wilaya zaidi ya 62. Huku serikali ikishusha ada kwa wanafunzi wanaosoma kozi za mwaka 1 – 3 kutoka shilingi 350,000 hadi shilingi 60,000 kwa wanafunzi wa kutwa n kutoka shilingi 600,000 hadi shilingi 120,000 kwa wanafunzi wanaosoma Bweni.
Elimu yetu sasa inakwenda kwenye maarifa ujuzi sio nadharia tena.
5. UMEME KWA VIJIJI 2,000 NA UUNGANISHO WA GRIDI YA TAIFA
Vijiji vilivyoishi gizani kwa miaka mingi – leo vina mwanga. Kigoma na Katavi wameachana na majenereta sasa wana umeme wa uhakika wa Gridi ya Taifa. Mradi wa umeme wa kupeleka umeme kwenye vitongoji umeanza.
Huu ni ushindi wa wakulima, biashara ndogo ndogo, walimu, watoto, viongozi wa dini, wafugaji, wanawake na vijana wote wa Tanzania.
6. UJENZI, UKAMILISHAJI NA UBORESHAJI WA BANDARI NA MELI KUNAKWENDA KUIFUNGUA ZAIDI NCHI YETU KIUCHUMI
Bandari za Tanga, Dar es Salaam, Mbambabay (Ziwa Nyasa) Mwanza na Kemondo Kagera(Ziwa Victoria), Kigoma (Ujiji,Kibirizi) na Kalema (Ziwa Tanganyika), Mtwara zimejengwa na kuboreshwa.
Ukamilishaji wa Meli mpya ya “New MV Mwanza” ambayo kwa sasa imeanza kutoa huduma ikisafiri kutoka Mwanza – Bukoba, Mwanza – Port Bel (Uganda) na Mwanza – Kisumu (Kenya). Aidha serikali imeingia mikataba ya kuanza ujenzi wa Meli mpya za abiria na mizigo ziwa Tanganyika.
Bandari kubwa ya uvuvi Kilwa imejengwa kuchochea shughuli za uvuvi. Hakika bahari imegeuka kuwa chanzo cha ajira na kipato.
7. BARABARA, MADARAJA NA MIUNDOMBINU KILA KONA
√Daraja la Tanzanite – Dar es Salaam
√Kigongo–Busisi (Magufuli) – Ziwa Victoria
√Wami – Pwani
√Pangani (Mto Pangani)
Barabara za Mabasi ya mwendokasi, Mradi wa DMDP Dar, barabara za ndani na barabara za zege hadi vijijini (ujenzi wa makalvati, madaraja madogo na makubwa – TARURA)
Miundombinu ya nchi hii inabadilika kila siku. Ujenzi hautulii – kasi ndiyo dira.
8. UWEKEZAJI MKUBWA – TANZANIA YA VIWANDA SIO NDOTO TENA
Tumevutia makampuni makubwa ya teknolojia:
√Elsewedy Electric (vifaa vya umeme)
√SATURN (uunganishaji wa magari)
√Kiwanda cha Vioo, Vigae, Saruji, bidhaa za chuma nk
√RYDER – nyaya za masafa marefu ya intaneti
√Kongani mpya ya viwanda 200 Kwala – SINOTAN na Elsewedy Kigamboni
√Viwanda vya sukari Bagamoyo, Kilombero (upanuzi), TPC (kusindika Molorses)
√ Viwanda vya uzalishaji wa mafuta ya kupikia ya alizeti kama Mainland nk
Tanzania inajenga uchumi wake si wa maneno, bali wa viwanda, teknolojia na ajira!
9. MRADI WA EACOP NA LNG – TANZANIA KATIKA RAMANI YA DUNIA
Bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga liko asilimia 60 kukamilika. Litaleta ajira na mapato ya kodi yanayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 2.3 kila mwaka.
Mradi mkubwa wa LNG Lindi utakaogharimu takribani shilingi trilioni 100 upo hatua za mwisho za mazungumzo ili uanze. Huu unatajwa kuwa utabadilisha kila kitu ‘Game changer’ wa uchumi wa Tanzania.
10. UHURU WA WATU – HAKI NA AMANI ZIMELINDWA
Leo Watanzania wana uhuru wa kuabudu, kufanya biashara, kusafiri ndani ya nchi, kuwekeza, kumiliki mali na kufurahia maisha bila kuogopa. Hii ndiyo Tanzania tuliyoirithi na tunayoitaka yenye amani na ulinzi wa haki za wananchi wake.
Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama simameni imara kushinda changamoto iliyojitokeza ya utekaji na watu kupotea kwani imejenga hofu. Tunawaamini mna weledi wa kutosha kukabiliana nayo!
SWALI LINAIBUKA…
Tanzania hii tunayoiona ikipaa kimaendeleo kwa kasi na nuru ya matumaini ndiyo tunataka kuichezea, kuikwamisha na kuivuruga?
Rais Samia Suluhu Hassan anayejenga uchumi, kufungua milango ya fursa na ajira, kuwalinda wanyonge na kurudisha heshima ya nchi ndiye tunayemshambulia maneno ya dhihaka, magumu na makali?
Hii siyo kawaida. Lazima tuwe macho. Dunia inatuangalia. Wapo watakaofurahia wakiona tumeharibikiwa. Wao watakua wamekamilisha azma yao watazawadiwa uraia na maisha mazuri ughaibuni. Sisi tutabakia tukijuta na mahangaiko. Nawakumbusha watanzania wenzangu Tanzania ni nyumba yetu tusikubali hata sekunde moja iharibikiwe.
MWISHO
Rais Samia ametuonesha njia. Sasa ni zamu yetu, tupande gari la maendeleo, tukamate fursa, tuijenge nchi yetu. Future ni yetu, Tumuunge mkono!


