Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Heslb) imesema wanafunzi 70,990 wa mwaka wa kwanza wamepatiwa mkopo wenye thamani ya Sh 233.3 bilioni kwa ajili ya muhula mpya wa masomo 2024/25.
Taarifa ya Dk Bill Kiwia, Mkurugenzi Mtendaji wa Heslb iliyotolewa Oktoba 21 inafafanua kuwa idadi hiyo imefikiwa baada ya kutangazwa kwa wanafunzi wengine 19,345 waliopangiwa mkopo katika awamu ya tatu.
“Heslb imetangaza awamu ya tatu (Batch Three) yenye wanafunzi 19,345 wa shahada ya awali waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh 59.49 bilioni kwa mwaka wa masomo 2024/2025,” imesema taarifa ya Dk Kiwia.
WANAFUNZI 19,345 WAPANGIWA MIKOPO YA TZS 59.49 BILIONI AWAMU YA TATU pic.twitter.com/FNM6gHXiWo
— HESLB Tanzania (@HESLBTanzania) October 20, 2024
Kati ya wanafunzi hao waliopata mkopo katika awamu zote tatu kwa msimu wa masomo 2024/25 wanaume 40,164 sawa na asilimia 56.5 na wanawake ni 30,825 sawa na asilimia 43.4.
Aidha, Heslb pia imesema imetoa mikopo kwa wanafunzi wapya wa stashahada 425 wakiwemo wa mwaka wa kwanza 378 na wanaoendelea na masomo 47.
Mikopo hiyo kwa ngazi ya stashahada ina thamani ya Sh1.1 bilioni huku wanafunzi wengine 599 wa mwaka wa kwanza wakinufaika na ruzuku ya ‘Samia Scholarship’ yenye thamani ya Sh 3 bilioni.