Vijana 500 wapewa siku 7 kuondoka mkoa wa Kilimanjaro baada ya kutapeliwa

HomeKitaifa

Vijana 500 wapewa siku 7 kuondoka mkoa wa Kilimanjaro baada ya kutapeliwa

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai, ametoa siku saba kwa vijana zaidi ya 500, wanaodaiwa kutapeliwa ajira na kampuni ya Alliance Motion in Global, mjini Moshi, kurudi makwao.

Kagaigai ametoa agizo hilo leo Jumatano, Septemba 15, 2021 wakati akizungumza na vijana hao ambapo amesema watakaokiuka agizo hilo na kuendelea kuwepo mkoani Kilimanjaro baada ya siku saba, watahesabika ni wahalifu na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu huyo pia alimuagiza Kamanda wa Polisi Kilimanjaro, kufuatilia mtandao wote uliohusika na utapeli huo kwa kuwahoji viongozi halali wa kampuni hiyo na watuhumiwa wafikishwe mahakamani haraka.

Vijana hao kutoka mikoa ya Mara, Tabora, Singida, Mbeya,Shinyanga, Kigoma na Tanga, wanadaiwa kutapeliwa ajira walizoahidiwa katika kampuni ya Alliance Motion in Global na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Joseph.Vijana hao wanadai kutozwa Sh200,000 hadi Sh900,000, na kuahidiwa kupewa ajira, kwa sasa wamepangishiwa vyumba katika kata ya Majengo na Njoro mjini Moshi na chumba kimoja wanakaa watu wanne huku wakidai kuishi mazingira magumu na hawana chakula.
Kigaigai amesema tukio hilo ni hatari kwa usalama na kumuagiza kamanda wa polisi kuwasiliana na makamanda wa polisi mikoa mingine ili kufuatilia mtandao huo unaojihusisha na utapeli huo hapa nchini.

“Ninyi mlikuwa mnashughulika na wezi na mmetapeliwa, poleni sana vijana, hakuna utaratibu wa mtu kuomba kazi na kuambiwa atume fedha kwanza na mimi ninachoelekeza rudini makwenu mlipotokea” amesema Kagaigai.
“Wote mlioitwa na kampuni hii walioko Kilimanjaro, ndani ya siku saba, muwe mmeondoka Kilimanjaro mrudi makwenu, mnaweza kuharibikiwa maisha na nisingependa hilo litokee, rudini nyumbani mkafanye kazi halali”
“Kwa kijana ambaye hataondoka, tutamchukulia ni  mzururaji na sheria ya uzururaji itafanya kazi yake, lakini niombe wakuu wa mikoa wenzangu hili wimbi ni baya, yawezekana pia lipo mikoa mingine, tushirikiane kulidhibiti hili” amesema
Amewataka Wenyeviti wa mitaa na watendaji wa Serikali za mitaa kurejea utaratibu wa zamani wa kuwahoji wageni wanaoonekana katika maeneo yao, ili kudhibiti matatizo kabla ya madhara.

“Wenyeviti wa mitaa na watendaji, naaomba tuanze ule utaratibu wa zamani, ambapo alikuwa akionejana mtu hafahamiki, alikuwa akihojiwa na taarifa kutolewa kwa uongozi wa juu, sasa Kilimanjaro ni lazima turudi huko, tukiona wageni tuwahoji na tukipata shaka tuende zaidi hadi polisi” Akizungumza mmoja wa vijana hao, anatokea Mkoa wa Mara, Stephano Chacha, amesema wanaishi mazingira magumu na kwa sasa hawana chakula.

“Wakati tunakuja niliambiwa nije na Sh250,000 na baadae nilipofika walimpigia baba yangu simu kumwambia kuwa nimefaulu vizuri, atume Sh600,000 kwa ajili ya kutumiwa vifaa mbalimbali na kompyuta na hela ile ikatumwa,” amesema
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema wanaendelea kuwashikilia watu sita na msako unaendelea kumtafuta mmiliki wa kampuni hiyo.

“Yapo madai kuwa watu hawa baada ya kubanwa Kilimanjaro, wamekimbilia mikoa mingine, na kwa mujibu wa taarifa wamekimbilia Singida, Mbeya na mikoa mingine, niombe makamanda wenzangu, tusaidiane na kupeana taarifa za kundi hili linalotapeli watu kwa mgongo wa kuwapa ajira” amesema.

error: Content is protected !!