MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Nyambi Athuman amesema endapo wananchi watamchangua kuwa mbunge wao atasimamia utekelezaji wa Ilani ya chama chake yenye maeneo 13 ya vipaumbele.
Maeneo hayo ya vipaumbele ni pamoja na uboreshaji wa huduma za afya, elimu, maji na miundombinu ambayo ni maono ya kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ifikapo mwaka 2030.
Mgombea wa ubunge huyo alisema hayo katika mkutano uzunduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu uliofanyika eneo la Soko la Mawenzi, Manispaa ya Morogoro.
Alisema CUF inaamini katika falsafa ya ‘Haki Sawa kwa Wote’ inahakikisha kila mwananchi anapata haki zake za kiuchumi, kijamii, mazingira bora na kipato cha msingi. Mgombea huyo alisema katika ilani hiyo imeelekeza kuboresha afya njema hususani kwa akina mama wajawazito na watoto kwa kupatiwa huduma bure, ustawi wa jamii, elimu bora kuanzia awali hadi chuo kikuu na jumuishi, kusimamia usawa wa kijinsia na haki za kundi maalumu.