Idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu itaongezeka kutoa 245,314 mwaka 2024/2025 hadi wanafunzi 252,773 mwaka 2025/2026.
Tarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda jana wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 bungeni Dodoma.
Profesa Mkenda alisema watakaopata mikopo hiyo mwaka 2025/2026; 88,320 ni wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea ni 164,453.
Alisema serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 10,000 wa ngazi ya stashahada katika fani za kipaumbele ikiwamo sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
“Itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi 2,630 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kupitia Samia Scholraship ambapo kati ya hao wanafunzi wa mwaka wa kwanza 1,220, shahada za umahiri 80 na wanafunzi wanaoendelea 1,330” alisema Profesa Mkenda.
Aidha, Profesa Mkenda alisema Serikali itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 50 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi hususani wa kike waliohitimu mitihani ya kitaifa ya kidato cha sita na shahada za awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).