Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damas Ndumbaro amesema watoa huduma kwenye sekta ya utalii nchini wanatakiwa kupata chanjo ya Korona (UVIKO-19) kwani itasaidia kujikinga na kujenga ujasiri wa watalii kuja kutembelea vivutio vya utalii na wao kufaidika na shughuli hizo.
“Wanaotoa huduma ambao hawajachanjwa wapo hatarini zaidi kupoteza maisha yao kwa vile wanakutana na watu wa kutoka mataifa mbalimbali duniani hususani yale ambayo yana maambukizi makubwa ya Uviko-19. Nawasihi kwa usalama wa maisha yao wachanje” amesisitiza Dkt Ndumbaro.
Licha ya kuimarishwa kwa tahadhari katika vituo vya utalii ikiwemo uvaaji barakoa, unawaji mikono, kutumia vitakasa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima lakini kwa sasa chanjo ni muhimu zaidi kwani tangu Serikali ya Tanzania iliporidhia kupokea chanjo watalii wameanza kuingia nchini sababu nchi inafuata maelekezo ya wataalamu wa afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO).
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini ametoa maagizo hayo jana Oktoba 16, 2021 wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Umoja wa Ulaya uliowakutanisha wadau mbalimbali wa utalii nchini kujadili changamoto mbalimbali zinazowikabili sekta ya utalii nchini.