Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo ametangaza kukamilika kwa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha.
Majaliwa amepongeza washiriki wote wa zoezi hilo na kuwataka wananchi kuepuka taarifa hasi za upotoshwaji kuhusu eneo hilo. Amesema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa nia njema ya kuhifadhi eneo hilo na kuwa hakuna wananchi wowote waliohamishwa katika eneo hilo.
“Eneo hili ni muhimu kwa kuwa na vyanzo vya maji na mazalia ya nyumbu ambayo ni muhimu kwa uwepo wa maeneo ya hifadhi za Serengeti na Ngorongoro”, alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu amebainisha kuwa eneo hili litaendelea kulindwa kwa wakati wote ili kuhifadhi eneo hilo ambalo ni muhimu kwa uhifadhi kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Pindi Chana alisema kuwa wizara na taasisi zilizo chini yake wataendelea kusimamia maeneo yote ya uhifadhi kwa niaba ya wananchi.