Kubenea apigwa spana kesi ya Makonda

HomeKitaifa

Kubenea apigwa spana kesi ya Makonda

Maombi ya mwanahabari Saed Kubenea ya kumfungulia mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinonondi yamewekwa mapingamizi  na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) na Mkuu wa Upelelezi Makosa ya Jina (DCI). 

Wakili wa Saed Kubenea, Hekima Mwasipu aliyataja mapingamizi hayo manne na kuyaelezea.

“Mapingamizi yako manne, pingamizi la kwanza linasema Kubenea hana maslahi na hii kesi. Pili wanasema Mahakama haina mamlaka ya kuyasikiliza. Tatu wanasema wakati tukio (Makonda kuvamia Ofisi za kampuni ya Clouds Media), Machi 17,2017, sheria tuliyotumia kuleta maombi haikuwa na nguvu kwa wakati huo , na la mwisho walisema maombi yote yaliyoletwa katika mahakama hii yalitokana na habari za kusikia,” alisema Wakili Mwasipu.

Kubenea aliwasilisha maombi ya kumfungulia mashtaka Makonda kwa kosa matumizi mabaya ya madaraka baada ya kuvamia Ofisi za kampuni ya Clouds Media mwezi Machi 17 mwaka 2017.

Hakimu Aron Lyamuya ametoa siku 14 kwa Jamhuri kuwasilisha hoja za mapingamizi kwa maandishi ifikapo Aprili 8 mwaka huu na upande wa waleta maombi wawasilishe majibu ya mapingamizi hayo kwa maandishi Aprili 22. 

 

error: Content is protected !!