Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amesema kuwa chama chake hakitachukua Sh110 milioni za ruzuku ya Serikali kwa sababu kwa kufanya hivyo watakuwa wanahalalisha matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Mbowe ameyasema hayo katika kitovu cha biashara cha Kariakoo ambapo alisema ni vyema watembee kwa miguu ili kuhamasisha watu kuchangia chama badala ya kuchukua ruzuku.
Mbowe ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 20, 2022 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Mtaa wa Raha Kariakoo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya ‘Jiunge na Mnyororo’ yenye lengo la kuhamasisha wananchi mbalimbali kuchangia chama.
Mbowe ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 20, 2022 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Mtaa wa Raha Kariakoo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya ‘Jiunge na Mnyororo’ yenye lengo la kuhamasisha wananchi mbalimbali kuchangia chama.
“Tulitakiwa kupata Sh milioni 110 kila mwezi, lakini chama kimekataa kwa sababu tukikubali tutahalalisha kilichotokea 2020,” alisema.
Aliongeza: Huu ni uamuzi mgumu wa kisiasa lakini hakuna namna na huu ni msimamo wa Chadema, ambao wakati mwingine unatupa shida sana. Binafsi nimeumizwa kwa namna mbalimbali kuhusu misimamo.
Mbowe ambaye kwa nyakati tofauti alishangiliwa na wafanyabiashara hao wakati akitoa hotuba yake, alisema iwapo siku Chadema itabadilisha msimamo wake basi ni hakika kuna jambo linashughulikiwa.
Katika kampeni ya ‘Jiunge na Mnyororo’ eneo la Kariakoo, wafanyabiashara na wananchi mbalimbali waliokuwa wakifuatilia mkutano huo walichangia fedha taslimu takriban Sh milioni moja.
Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai, mkoani Kilimanjaro amesema ajenda ya Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 iko hai, akisema watawaamsha Watanzania kuidai.