Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA), imeonya kuwa watumiaji wa dawa za kuongeza nguvu za kiume pasi na maelekezo ya wataalamu wa afya wako hatarini kupoteza maisha kutokana na dawa hizo kuwa na sifa ya kupanua mishipa ya damu.
Tahadhari hiyo ilitolewa jana na Mkurugezni Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo, alipotoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya dawa hizo wakati wa semina kwa wahariri wa habari iliyoandaliwa na mamlaka hiyo jijini Mbeya.
“Watu wanakufa kwenye nyumba za kulala wageni kutokana na matumizi holela ya dawa hizi. Ufuatiliaji wetu kwenye maduka ya dawa umeonyesha dawa hizi sasa zinaongoza kwa kununuliwa zaidi nchini. Zitumike kwa ushauri wa daktari tu,
“Kwa hiyo, baadhi ya wazalishaji wa dawa walitumia nafasi hiyo kutengeneza dawa hizo za kuongeza nguvu za kiume. Shida ya hizi dawa ni kwamba zinasababisha kupanuka kwa mishipa ya damu. Mishipa ya damu iliyoko kichwani ikipanuka, mtu anakufa,” alisema Dk. Fimbo.
Aidha. Dk. Fimbo alisisitiza kwamba dawa hizo zinapaswa kutumiwa na mtu aliyethibitika kitaalamu kutojimudu kwenye tendo la ndoa, lakini matumizi yake kikiwamo kiwango cha dozi,lazima yaidhinishwe na daktari.