Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Haruna Lipumba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi vizuri tangu aingie madarakani, kwa kukutana na viongozi wa siasa kama njia moja wapo ya kuendeleza demokrasia na pia kumhakikishia kwamba endapo ataendelea na utendaji wake huu wa kazi basi ana nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2025.
“Ombi langu, katika uchaguzi unaokuja 2025, tusirejee kwenye kile ambacho Rais kikwete alikiita sunami la ya 2020. Tufanye uchaguzi ulio huru na wa haki, na kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuleta maendeleo kwa watanzania, naamini kabisa ukishiriki uchaguzi wa 2025, uchaguzi ukawa wa huru na wa haki una nafasi nzuri tu ya kuweza kushinda uchaguzi huo,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Mkoani Tabora leo Mei 19,2022, Profesa Lipumba pia amepongeza tena Mhe. Rais Samia kwa kuendeleza demokrasia nchini tangu aingie madarakani.
“Mheshimiwa Rais hotuba yako uliyoitoa kwenye Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania ilitupa matumaini makubwa, matumaini ya maendeleo kwa upana wake, ulieleza hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi hii ukasisitiza demokrasia ni nyenzo yakuleta maendeleo,”- Profesa Lipumba.
Aidha, Profesa Lipumba amempa moyo Rais Samia na kumwambia ajiwekee lengo la kushinda tuzo za kuheshimu demokrasia, haki za binadamu na pia kuletea maendeleo kwa wananchi wa Tanzania.