Siku ya jana Ijumaa Mei 20,2022 Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kilichopo jijini Dar es Salaam kiliwaka moto ambao uliteketeza baadhi ya vifaa katika ofisi zilizopo chuoni hapo ikiwemo ofisi ya chama cha wanataaluma.
Mratibu wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Ilala, Elisa Mugisha alisema bado chanzo cha moto huo hakijafahamika ingawa waliwahi kuuzima.
“Tulitoka kwa muda mfupi na ilipofika saa 7:42 mchana tukawa tumeanza kazi ya kuzima moto huo uliokuwa unawaka sehemu ya chini ya ghorofa, eneo hilo lina ofisi mbalimbali, ikiwemo chama cha wanataaluma, Saccos na kasijala,” alisema Mugisha.
Mugisha alisema walipambana na moto ndani ya muda mfupi, ukawa umezimika na hakuna madhara yoyote kwa binadamu na kueleza kinachofuata ni uchunguzi ili kujua chanzo cha moto huo.
Mashuhuda wasimulia
Jamson Siwa ambaye ni mfanyabiashara katika maeneo ya chuo hiko, alisema moto huo ulizua taaruki kwa sabbabu ulianza kwa kutoa moshi mwingi eneo la chini la jengo hilo karibu na mgahawa wa chuo hicho.
“Ulianza kama moshi, kwahiyo ungeweza kufikiri labda ni jiko la mgahawa wanachoma nyama, kadri muda ulivyozidi kuyoyoma mambo yakabadilika, tukaona moto ukitokea ila umechoma sehemu ndogo ya chuo hicho,” alisimulia Jamson.
Naye Hellen Michael mwanafunzi wa chuo hicho alisema: “nilikuwa katika sehemu ya kyla chakula, nikaanza kuona moshi unatoka na baadaye moto ukawaka, lakini sijasikia taarifa kutoka katika uongozi wa chuo kama kuna mtu amedhurika,” alisema Hellen