Ukweli kuhusu wakazi wa  Ngorongoro

HomeKitaifa

Ukweli kuhusu wakazi wa Ngorongoro

Serikali  imesema wananchi wa maeneo ya Loliondo wapo salama ikibainisha kuwa “hakuna mapambano yoyote” kati ya polisi na wakazi hao wa kaskazini mwa Tanzania. 

Kauli hiyo ya Serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dodoma imekuja baada ya Spika wa Bunge la Tanzania Dk Tulia Ackson kuitaka Serikali ieleze juu ya video inayosambaa mitandaoni ikionyesha wananchi wa Loliondo wakitaka kupambana na watu wanaosemekana ni askari.

Katika majibu yake, Majaliwa amesema Serikali ilikubaliana na wanavijiji wa vijiji 14 vya eneo la Loliondo kutunza eneo ambalo ni mazalia ya wanyama, njia na chanzo cha maji na tangu juzi walianza kuweka alama zitakasaidia wakazi na Serikali kuamua mwisho wa eneo la malisho. 

“Alama hizi sio wigo lakini ni alama inayoonesha kwamba unapofika hapa kama unataka kulisha ukifika huku ni kwenye chanzo cha maji,” amesema Majaliwa. 

Hakuna mkazi atakayehamishwa

Majaliwa amewaambia wabunge kuwa zoezi hilo halimuondoa mtu yeyote anayeishi kwenye eneo lile, vijiji vitaendelea kubaki na hadhi yake na shughuli za wananchi zitaendelea kuwepo huku wakazi hao wa vijiji 14 na Serikali wakiendelea kulitunza eneo hilo. 

Akielezea undani wa video hizo, Majaliwa amesema hakuna mapambano yoyote yanayoendelea katika eneo hilo na kusema kuwa video hiyo inayosambaa mitandaoni ni upotoshaji kwa kuwa Serikali imeendelea kuratibu zoezi la uhifadhi wa eneo la Loliondo kwa kuwashirikisha wenyeji wa eneo hilo. 

Amesema  Juni 9, kulikuwa na mkutano katika kijiji cha Ololosokwan uliotishwa katika eneo hilo ambapo kulikuwa na baadhi ya kundi la watu wanaopinga jitihada hizo za uhifadhi. 

“Wakaanza kutengeneza video na wale waliokuwa wanahamasisha ili kuonesha kwamba kuna tatizo huko lakini hakukuwa na kundi lolote la askari ambalo lilikuwa likitaka kufanya kitendo chochote kibaya dhidi yao,” amesema kiongozi huyo leo (Juni 10, 2022). 

“Walikuwa wao wenyewe tu wakifanya majaribio yani kama vile wanatishia ili wapige picha wazirushe ioneshe kama Loliondo kuna tatizo na ndio sababu kwenye video ile huoni kama kuna askari yeyote anatishiwa mshale,”  ameongeza Majaliwa. 

Maigizo hayo, amesema yalilenga kujenga taswira hasi ndani na nje ya nchi kuwa kuna shida huko Loliondo. 

Tangu jana jioni kumekuwa na video zinazosambaa mitandaoni zikionyesha baadhi ya wakazi wakikimbia huko na huko zikiwa na maelezo kuwa ni mapambano yanayoendelea huko Liliondo. Hadi sasa Nukta Habari haijathibitisha bayana juu ya ukweli wa video hizo.

Wapotoshaji waonywa

Waziri Majaliwa amewaonya baadhi ya wapotoshaji ambao wametengeneza video hiyo kuonesha kuwa wananchi wa eneo hilo wakipambana na askari.

Aidha Dk Ackson ameishauri serikali kuwafuatilia wapotoshaji hao ambao wamekuwa wakizua taharuki kwa wananchi.

 

SOURCE : NUKTA HABARI

error: Content is protected !!