15 wafutiwa matokeo kidato cha 6

HomeElimu

15 wafutiwa matokeo kidato cha 6

Watahiniwa 15 wamefutiwa matokeo yao ya mtihani wa kidato cha sita Mwaka 2022 kutokana na vitendo vya udanganyifu idadi ambayo imepungua kwa takriban mara mbili ndani ya mwaka mmoja.  

Katika mkutano wake na wanahabari, Naibu Katibu wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) Athumani Amas amesema robo tatu ya watu hao ni watahiniwa wa shule. 

Uamuzi huo wa Necta utawapelekea maumivu watahiniwa hao kwa kuwa sasa utawafanya wakose fursa ya kuendelea na masomo ya juu mwaka huu.

“Baraza la mitihani katika mkutano wake limefuta matokeo yote ya watahiniwa 15, waliobainika kufanya vitendo vya udanganyifu katika mtihani, kati ya watahiniwa hao 13 ni watahiniwa wa shule na wawili ni watahiniwa binafsi,” amesema Amas wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita pamoja na ualimu mwaka 2022.  

Katika matokeo ya mwaka 2021, wanafunzi 27 walifutiwa matokeo yao kutokana na vitendo vya udanganyifu. Hii ina maana kuwa angalau mwaka huu idadi ya watahiniwa wadanganyifu imepungua kwa takriban asilimia 52. 

Hata hivyo, bosi huyo wa Necta hakueleza kwa undani vitendo ambavyo wamefanya watoto hao. Miongoni mwa vitendo maarufu vya udanganyifu katika mitihani ni kuingia na karatasi za majibu au simu kwenye chumba cha mtihani au kuangalizia mtihani wa mwenzio. 

Amas ametoa pongezi kwa kamati za uendeshaji wa mitihani kwa kuzingatia na kusimamia kikamilifu sheria na taratibu za uendeshaji mitihani na hivyo kuzuia udanganyifu.

Sanjari na uamuzi huo, baraza hilo lenye makao yake Mikocheni jijini Dar es Salaam, limezuia matokeo ya watahiniwa 21 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani kwa baadhi ya masomo.

Kwa mujibu wa Amas, watahiniwa husika ambao hawakufanya mitihani hiyo kwa sababu ya maradhi wamepewa fursa ya kufanya mitihani Mei 2023 kama watahiniwa wa shule.

error: Content is protected !!