Kampuni ya Kimataifa ya huduma ya Kontena Tanzania (TICTS) inadaiwa kushindwa kutekeleza makujukumu yake na wadau wa sekta za biashara na usafirishaji ambao wameitaka serikali kutoipa mkabata mpya kampuni hiyo kwa kushindwa kufikia lengo la kuongeza wingi wa mzigo kwa asilimia 37 kwa mwaka.
Wadau hao wameeleza kwamba kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa TICTS, kumesababisha ucheleweshaji wa mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam na kulikosesha taifa mapato kutokana na wafanyabiashara kuamua kuikwepa bandari na kukimbilia Kenya, Afrika kusini na Namibia zenye ufanisi.
Takwimu zinaonyesha kwamba TICTS walihudumia makontena ya futi 21 (TEUs) 606,169 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.8 kulinganisha na mwaka 2020 hivyo kushindwa kufikia lengo la kimkataba la kuongeza mzigo wa kontena kwa asilimia 37 kwa mwaka mmoja.
Wadau hao wamesema pia kwamba, kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa TICTS imefanya bandari ya Kenya kuwa kitovu yenye kupitisha makontena ya TEU milioni 2 kwa mwaka huku bandari ya Durban nchini Afrika Kusini ikijipanga kuongeza ufanisi hadi kufikia TEU milioni 11 ndani ya miaka michache ijayo.
Wabia wa TICTS ni pamoja na waziri wa zamani Nazir Karamagi na mfanyabiashara maarufu Yogesh Manek, wakishirikiana na mwekezaji wa nje, kampuni ya Hutchinson Ports ya Hong Kong.
John Tarimo, mfanyabiashara wa Dar es Salaama anayeagiza bidha kutoka China alisema serikali isiwape TICTS mkataba mpya tena kwani wameshindwa kufanya kazi kwa miaka 20 sasa na hivyo tenda hiyo ipewe kampuni nyingine itakayoweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan ametoka kulalamika kuhusu ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam hivyo akamtengua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Eric Hamissi na nafasi yake kumpa Plasduce Mbossa ambaye aliahidi kuongeza kufanisi wa bandari.