Juni 8,2021, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alionyesha wazi imani yake kubwa kwa wanawake na nia yake ya kuwainua kwa kile alichokiamini kwamba wanauwezo mkubwa wa kuleta maendeleo katika nchi.
Alikiri kwamba wanawake ni jeshi kubwa ambalo linategemewa katika uchumi na ustawi wa jamii hivyo hawapaswi kubaki nyuma na badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo kufanya mageuzi yatakayolisaidia Taifa kusonga mbele.
Wanawake wamekua wakijishughulisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili waweze kuendesha maisha yao ya kila siku ambapo baadhi ya kazi zao zinawazalimu kutumia nishati hatarishi zenye madhara na kuwaathiri afya zao pamoja na mazingira yao.
Katika kuhakikisha juhudi za Rais Samia za kuwawezesha wanawake hasa kutoka kaya masikini wanawezeshwa, Waziri wa Nishati, January Makamba akiwa kwenye ziara yake ya mikoa 14 kuangalia shughuli zinazotekelezwa na taasisi zilizo chini ya wizara yake na kupokea maoni na kero za wananchi, amegawa bure mitungi ya gesi kwa kina mamalishe.
Lengo la kugawa bure mitungi hiyo ya gesi safi ni kuhakikisha wanawake hao wanaondokana na changamoto za kutumia kuni na mkaa kupikia, hali inayochangia madhara ikiwemo moshi unaosababisha maumivu ya kifua, kichomi na magonjwa ya upumuaji.
Mitungi ya gesi zaidi ya 1,200 imeshagaiwa kwa kina mama na kaya masikini za mikoa ya Kagera, Simiyu, Mwanza na Mara, amekuwa akiwafuata mamalishe kwenye maeneo yao ya kazi ili kuhamasisha wengine kutumia nishati hiyo.
Kwa kuwazesha wanawake hawa, itawasaidia kufanya kazi zao kwa uharaka zaidi na kwenda kujishughulisha na katika shughuli nyingine za kijamii zitakazoweza kusaidia kuchangia kwenye pato la taifa.