Watumiaji wa usafiri wa anga waongezeka

HomeKitaifa

Watumiaji wa usafiri wa anga waongezeka

Idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga nchini Tanzania imeongezeka kwa asilimia 38 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, baada ya kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Uviko-19.

Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi kwa mwaka 2021 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya abiria waliotumia usafiri wa anga nchini mwaka 2021 walikuwa milioni 3.8 wakiongezeka kutoka milioni 2.7 wa mwaka 2020.

Hilo ni sawa na ongezeko la abiria milioni 1.1 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kati ya abiria hao, milioni 2.3 sawa na asilimia 60.5 walikuwa abiria wa ndani.

Tangu mwaka 2017 hadi 2021 idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga nchini imekuwa ikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kusitishwa kwa muda kwa safari za ndege mwaka 2020 kutokana na janga la Uviko-19.

Mathalan, Mwaka 2017 abiria waliotumia usafiri huo walikuwa milioni 5 na mwaka uliofuata waliongezeka hadi milioni 5.1 kabla hawajaongezeka zaidi hadi milioni 5.4.

Hata hivyo, mwaka 2020, idadi hiyo ilishuka mara mbili hadi milioni 2.7.

“Kutokana na katazo la safari za anga kufuatia mlipuko wa Uviko-19, jumla ya mashirika 21 ya kimataifa ya ndege yalifuta safari 632 zilizopangwa kufanyika kuja nchini kuanzia tarehe 20 Machi 2020,” imeeleza sehemu ya kitabu hicho.

Hatua hiyo ilisababisha kudorora kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi hususan biashara na huduma kama usafirishaji wa chakula, vinywaji na burudani.

Baada ya hatua mbalimbali kuchukuliwa kukabiliana na Uviko-19 ikiwemo utoaji wa chanjo na kulegezwa kwa masharti ya safari za kimataifa, kumesaidia sekta ya anga kuimarika siku za hivi karibuni.

Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kuwa Serikali imedhamiria kuhuisha shughuli za usafiri wa anga nchini ikiwemo Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kujiendesha kibiashara na kulipunguzia mzigo wa madeni.

Mpaka sasa, Serikali ina ndege 11 zinazofanya safari za ndani na nje ya nchi ambapo mwaka huu wa 2022/23 ina mpango wa kufanya ununuzi wa ndege nyingine tano ili kuongeza ufanisi wa shirika hilo.

Ndege zitakazonunuliwa: moja ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, ndege mbili ni aina ya Boeing 737-9, ndege moja ya mizigo aina ya Boeing 767-300F na ndege moja aina ya Dash 8 Q400.

Huenda ujio wa ndege hizi utaongeza ushindani katika sekta ya anga nchini na hivyo kuongeza idadi ya abiria wanaotumia usafiri wa anga ili kuingizia Serikali mapato mengi zaidi.

error: Content is protected !!