Kama ulikuwa hujui mikoa inayoongoza kwa watumiaji wengi wa simu za mkononi, basi Dar es Salaam inashika namba moja katika orodha ya mikoa 10 yenye watumiaji wengi wa kifaa hicho cha mawasiliano.
Matumizi ya simu hupimwa kwa idadi ya watu waliojisajili kutumia mitandao ya simu za mkononi na mezani inayotoa huduma hiyo nchini ya Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL, Halotel na Smile.
Uchambuzi wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2022 (Aprili-Juni 2022) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaongoza kuwa na idadi kubwa ya watu wanaotumia simu Tanzania.
Ripoti hiyo inayopatikana katika tovuti ya TCRA, inaeleza kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu, mkoa huo uliopo mashariki mwaka Tanzania ulikuwa na watumiaji wa simu milioni 9.1 sawa na asilimia 16.2 ya watumiaji wote simu milioni 56.2 waliorekodiwa Juni.
Hiyo ni sawa na kusema kwa kila watu 100 wanaotumia simu Tanzania, basi 16 wapo Dar es Salaam.
Pia uchambuzi zaidi wa takwimu hizo za mawasiliano, unaonyesha kuwa idadi ya watumiaji simu wa Dar es Salaam ni zaidi ya mara 48 ya watumiaji waliopo kisiwa cha Pemba, Zanzibar chenye mikoa miwili ya Pemba Kaskazini na Pemba Kusini.
Mikoa ya Pemba ndiyo yenye watumiaji wachache zaidi wa simu za mkononi nchini Tanzania. Juu kidogo ya Pemba kiko kisiwa cha Unguja chenye watumiaji wa 414,763 kikifuatiwa na Mkoa wa Katavi kwa watumiaji 658,809.
Dar es Salaam inafuatiwa kwa mbali na Mkoa wa Mwanza uliokuwa na watumiaji milioni 3.4 ukishika nafasi ya pili. Nafasi ya tatu imeeleza kwa Mkoa wa Arusha (milioni 3.3) na Tabora katika nafasi ya nne ikiwa na watumiaji wa simu milioni 3.
Namba tano imeenda kwa Mkoa wa Mbeya ambao kwa mujibu wa TCRA hadi Juni 2022 ulikuwa na watumiaji wa simu milioni 2.9 ukifuatiwa na Morogoro (milioni 2.9), Dodoma (milioni 2.8) na Kilimanjaro milioni 2.7.
Nafasi ya tisa imeenda kwa Tanga ambao ulikuwa na watumiaji wa simu milioni 2.1 na 10 bora imefungwa na Mkoa wa Geita kwa watumiaji milioni 2.1.
Mikoa hiyo 10 inaunda jumla ya watumiaji wa simu milioni 34.4 ambao ni sawa na asilimia 61.3 ya watumiaji wote waliokuwepo hadi Juni mwaka huu.
Katika orodha hiyo pia mikoa yenye majiji sita ya Tanzania imefanikiwa kuingia katika orodha hiyo, jambo linaloweza kudhihirisha kuw aidadi ya watu katika mkoa husika inachangia uwepo wa watumiaji wengi wa simu.
Mathalan, Mkoa wa Dar es Salaam ambao una watu wengi zaidi Tanzania ndiyo unaongoza kuwa na watumiaji wengi wa simu nchini.
Watumiaji wazidi kuongezeka
Kwa mujibu wa TCRA idadi ya watumiaji wa simu inazidi kuongezeka kila mwaka ambapo hadi kufikia mwaka unaoishia Juni 2022, Tanzania ilikuwa na watumiaji milioni 56.2 kutoka milioni 53.2 waliokuwepo kipindi kama hicho mwaka jana.
Huenda idadi ya watumiaji ikaendelea kuongezeka kila mwaka kutokana na ongezeko la watu na mahitaji ya mawasiliano ya simu.
SOURCE : NUKTA HABARI