Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemsimamisha Kazi Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijini RUWASA wilaya Karagwe, Mhandisi Magai Kakuru kwa kushindwa kusimamia miradi ya Maji inayoendelea kutekelezwa Wilayani Karagwe.
Ametoa agizo hilo jana septemba 11, 2022 wakati alipoambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Innocent Bashungwa kukagua mradi wa maji wa Chanika/Omululama ulipo wilayani humo na kutoridhishwa na hali ya utekelezaji wa mradi huo.
“Mhandisi huyu anajitahidi kufanya kazi lakini haiendani na kasi inayohitajika kwahiyo ataenda kusaidia kwenye kazi nyingi, hapa karagwe nitaleta Meneja Mwingine anayeendana na kasi tunayoitaka” amesema Aweso
Waziri Aweso amesema alipokuja wilaya karagwe alitoa maelekezo mahususi kuhusu miradi ya maji, lakini jana baada ya kuona na kupata taarifa amegundua wakandarasi wanachezea fedha za miradi.
Aidha, Aweso ameagiza Mkandarasi ayetekeleza mradi wa maji wa vijijini nane wilayani Karagwe nae aondolewe na mchakato wa kupata Mkandarasi Mwenye Uwezo na atakayetekeleza miradi ya maji ndani ya muda wa mkataba.