Hatimaye mara baada ya kusubiri kwa muda mrefu wabunge tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (Eala) wamepatikana na kutangazwa na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson.
Wabunge hao wametangazwa kufuatia uchaguzi uliofanyika jana Septemba 22, 2022 bungeni jijini Dodoma ambapo awali wagombea 20 walinadi sera zao kwa wabunge 322 wa Bunge la Tanzania kwa lugha ya Kiingereza ili wapigiwe kura.
Wabunge hao tisa wametoka katika makundi manne yaliyopigiwa kura ambayo ni wanawake lililotoa wabunge watatu, Tanzania bara (3), Zanzibar (2) na vyama vya upinzani mmoja.
Kundi la wanawake wagombea waliochaguliwa ni Angela Kizigha aliyepata kura zote 322, Nadra Mohammed aliyepata kura 310 pamoja na Shogo Mlozi aliyepata kura 322.
Dk Abdullah Makame amechaguliwa kwa kupata kura 305 pamoja na Machano Ali Machano aliyepata kura 291. Wawili hawa wanawakilisha kundi la wagombea wa Zanzibar.
Katibu wa Bunge Nenelwa Mwihambi aliendelea kutaja matokeo ya kundi tatu lililokuwa na wagombea wa vyama walio wachache Bungeni ambapo Mashaka Ngole aliibuka mshindi kwa kura 234 akiwabwaga Ado Shaibu pamoja na Jafar Mneke.
Washindi katika kundi la nne la wagombea wa Tanzania bara ni Ansar Abubakar Kachwamba aliyepata kura 300, James Kinyasi (kura 312) pamoja na Dk Ngwaru Jumanne Maghembe aliyepata kura 311.
Mara baada ya Katibu wa bunge kumaliza kusoma matokeo hayo Spika Tulia Akson aliwatangaza washindi hao tisa akiwapongeza na kuwataka kuiwakilisha nchi vyema.
“Tumewachagua sisi leo kwa niaba ya wananchi wote kwenda kutuwakilisha sisi kama Watanzania kwenye Bunge la Eala na tunawategemea mnapoenda kule si hoja ya mawazo yenu ni hoja ya nchi na tunaamini mtaenda kuwakilisha nchi yetu,” alihitimisha Dk Tulia huku akipigiwa makofi na Wabunge.
Wawakilishi wa Eala hupigiwa kura kila baada ya miaka mitano katika mabunge ya nchi zao na uchaguzi wa mwisho ulikuwa mwaka 2017.
Hata hivyo, katika washindi hao tisa waliotangazwa watatu kati yao wanaendelea kushikilia nafasi zao kwani walikuwepo katika bunge lililopita akiwemo Dk Ngwaru Maghembe, Abdullah Makame pamoja na Angela Kizigha.